Na Mwandishi Wetu, MAELEZO
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki amezitaka kampuni binafsi nchini kuweka utaratibu maalum wa kuwasaidia wafanyakazi na familia zao pindi wanapokabiliwa na majanga mbalimbali ya kibindamu ikiwemo ajali na vifo.
Waziri Kairuki aliyasema hayo jana Jumatatu (Desemba 16, 2019) wakati wa ziara yake ya kutembelea Kampuni ya vinywaji baridi ya SBC Tanzania Ltd inayozalisha vivywaji vya Pepsi, Mirinda, Mountain Dew na 7up, na kusema utaratibu huo utasaidia kuongeza tija, motisha na uzalishaji katika makampuni hayo.
Waziri Kairuki alisema Kampuni ya SBC Tanzania imekuwa ni miongoni mwa makampuni machache nchini yaliyoweka utaratibu wa kusaidia wafanyakazi wake wakati wa majanga, ikiwemo vifo na hivyo kuwataka waajiri wa makampuni mengine kuiga mfano huo kwani wafanyakazi ni kiungo muhimu cha mafanikio ndani ya makampuni hayo.
‘Hapa PESPI kuna Mtumishi alifariki akiwa kazini, na kampuni ya SBC ilimchukua mtoto wake na kumuendeleza kielimu kuanzia degree (Shahada) ya kwanza hadi ya pili na yupo katika Idara ya Masoko ya kampuni hii na huu ni mfano mzuri unaopaswa kuigwa na makampuni mengine katika kuendeleza familia za wafanyakazi wao pindi wanapofariki’ alisema Waziri Kairuki.
Aidha Waziri Kairuki alisema kitendo cha kuweka utaratibu wa kuwasadia wafanyakazi na familia zao wakati wa majanga utasaidia kuendeleza kizazi kinachofuata ndani ya kampuni hizo na hivyo kuwafanya kufurahia kufanya kazi ndani ya kampuni hizo na kuhimiza utaratibu huo kuwa endelevu ili kuzidi kuimarisha ushirikiano baina ya kampuni hizo na familia za wafanyakazi.
Akizungumzia kuhusu uzalishaji wa Kampuni hiyo, Waziri Kairuki aliupongeza Uongozi wa SBC Tanzania Ltd kutokana na juhudi na jitihada kubwa inazoendelea kuzifanya katika kukuza soko la bidhaa za vinywaji nchini sambamba na kuendelea kutoa ajira kwa Watanzania na hivyo kuchangia katika kukuza uchumi nchini.
Akitolea mfano Waziri Kairuki alisema Kampuni hiyo yenye mtaji wa Dola Milioni 373 imeendelea kukuza mnyoyoro wa thamani wa bidhaa zake nchini, ambapo katika kipindi cha miaka 18 tangu kuanzishwa kwake kiwanda hicho kimeonyesha uhalisia wa kazi kubwa inayofanya, na hilo linadhihishwa na kiwango cha malipo ya kodi kwa Serikali ya Tsh Bilioni 416 iliyolipa kuanzia mwaka 2001.
‘Kampuni hii ilianza mwaka 2001 ikiwa wafanyakazi 76 na mtaji wa uwekezaji wenye thamani ya Tsh Bilioni 24.6, lakini kwa sasa ina jumla ya wafanyakazi walioajiriwa katika ajira ya moja kwa moja takribani 1215, na pia wameendelea kuhuisha mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wao kila baada ya miaka 2-3’’ alisema Waziri Kairuki.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya SBC Tanzania Ltd, Avinash Jha alisema Kampuni hiyo itaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na serikali katika kufanikisha mikakati mbalimbali ikiwemo sera ya uchumi wa viwanda, hatua inayolenga kuleta maendeleo jumuishi kwa Watanzania wote.
Jha aliongeza kuwa kampuni yake itaendelea kuzingatia sera, miongozo na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Serikali ikiwemo kutoa ajira kwa vijana wengi wa Kitanzania sambamba na kuwajengea uwezo na uzoefu wa kazi ili kumudu changamoto zilizopo katika soko la ajira nchini.
MWISHO