Na Mwandishi Wetu,MAELEZO
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kariuki amewataka wadau na makampuni ya sekta binafsi nchini kuendelea kutoa maoni na mapendekezo yao ya kitaalamu kuhusu Rasimu ya Sheria ya Uwezeshaji Biashara inayolenga kuweka mazingira wezeshi ya uimarishaji wa sekta ya biashara nchini.
Akizungumza na Menejimenti ya Wafanyakazi wa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) jana Jumatatu (Desemba 16, 2019), Waziri Kairuki alisema Serikali itaendelea kuwa mdau wa karibu na sekta binafsi na kutambua jitihada mbalimbali na kuendelea kuwaunga mkono katika kuchagiza shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Aidha Waziri Kairuki, alisema Serikali imekusudia kukusanya maoni mbalimbali ya wadau wake ili kuhakikisha itatunga Sheria imara itayosaidia kukuza na kuimarisha sekta ya biashara nchini, hivyo sekta binafsi ni wadau muhimu wanaopaswa kutoa mapendekezo, maoni na uzoefu walionao kwa kuzingatia aina ya biashara na mifumo ya kisheria iliyopo nchini.
Serikali imeamua kuja na Sheria mpya kabisa itayohusika na biashara peke yake na hili tutakusudia kuangalia ni maeneo yapi yanapaswa kuboreshwa ikiwemo masuala ya kisera, kisheria na kikanuni ili kuziweka katika eneo moja na pale kwenye changamoto tufanye marejeo na marekebisho’’ alisema Waziri Kairuki.
Kwa mujibu wa Waziri Kairuki Rasimu ya Sheria ya Uwezeshaji Biashara imekusudia kwenda sambamba na Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara Nchini (Blue Print) ambapo sekta biashara inatajwa kuwa kiungo muhimu katika ufanikishaji wa mikakati hiyo, hivyo Serikali inategemea kwa kiasi kikubwa maoni na mapendekezo yao katika kuweka mazingira wezeshi ya kuimarisha sekta ya biashara nchini.
Waziri Kairuki alisema Ili kuhakikisha Mipango na Mikakati iliyopo itaendelea kuimarisha na kukuza sekta ya biashara nchini, Serikali itaendelea kulinda viwanda vya ndani ili kuhakikisha kuwa mnyororo wa thamani sambamba kwa kuongeza kasi ya ununuzi wa malighafi sambamba na kupanua masoko ya bidhaa za ndani na nje ya nchi.
Aliongeza kuwa sambamba na kutunga Sheria ya Uwezeshaji Biashara, Serikali pia imeanza mchakato wa kutunga sheria ya Uwekezaji inayolenga katika kubainisha vikwazo na changamoto mbalimbali zinazowakabili wawekezaji nchini na hivyo kuwa na utaratibu utaowawezesha kuwa na mazingira wezeshi na kuvutia wawekezaji wengi zaidi wa ndani na nje ya nchi.
‘Hapa katika Sheria hii tumeamua kuja na mpango maalum wa kujua ni wapi One-Stop center iwepo, nini kinahitaji, changamoto za vibali pamoja na masuala mengione muhimu ambayo ni muhimu katika usimamizi kwa wawekezaji wetu nchini na kama mambo yatakaa vizuri katika Bunge lijalo tutaanza mchakato wake’’ alisema Waziri Kairuki.
Kwa upande mwingine Waziri Kairuki alisema Serikali itaendelea kuijengea uwezo Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) ili kuweka mkazo katika shughuli za utafiti na ubunifu na kuhakikisha kuwa viwanda vya ndani vinaendelea kuwa na wataalamu imara watakaokidhi viwango, sifa na vigezo zinahitajika.
Akizungumzia kuhusu uzalishaji wa kiwanda cha TCC, Waziri Kariuki alisema Serikali inaridhishwa na kasi kubwa ya uzalishaji unaofanywa na kampuni hiyo na kuitaka kuendelea kulinda maslahi ya Watanzania na kuwataka kutumia uzoefu wa wafanyakazi wa kigeni waliopo kiwandani hapo ili kuongeza ujuzi na maarifa kwa wafanyakazi wa Kitanzania ili katika miaka michache ijayo kampuni hiyo iwe na idadi kubwa ya Watanzania.
‘Kwa miaka 58 mmeendelea kufanya kazi nzuri, endeleeni kutoa motisha kwa Wafanyakazi wa Kitanzania, kama nilivyoeleezwa kuwa 71% ni Watanzania, tunahitaji siku za usoni utaalamu wa wageni hawa uweze kuhamia kwa Watanzania’’ alisema.
MWISHO
Social Plugin