Na Editha Karlo,Kasulu
WAZIRI wa Nishati Dk. Medard Kalemani, amesema uamuzi wa serikali kuzuia uingizwaji wa nguzo za umeme kutoka nje ya nchi na kuruhusu ujenzi wa viwanda vya kuzalisha nguzo hizo nchini umesaidia pakubwa kwa serikali kufikisha huduma ya umeme kwa wananchi wengi hasa walioko vijijini.
Waziri Kalemani, amesema hayo wakati akizindua kiwanda kuzalisha nguzo za umeme cha kampuni ya Qwihaya General Enterprises Co.Ltd, kilichojengwa katika Kata ya Heru Juu, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, chenye uwezo wa kuzalisha nguzo 700 kwa siku.
Amesema kwa sasa uzalishaji wa nguzo za umeme hapa nchini umefikia Milioni 3 wakati mahitaji ni Milioni moja na nusu, tofauti na ilivyokuwa miaka minne iliyopita ambapo mahitaji yalikuwa nguzo Milioni moja na laki mbili wakati upatikanaji wa nguzo ulikuwa ni laki nne tu, na kwamba mafanikio hayo yametokana na kuongezeka kwa viwanda vya kuzalisha nguzo hizo nchini, kutoka kiwanda kimoja mwaka 2015 hadi kufikia viwanda kumi mwaka huu.
Waziri Kalemani amesema siku za nyuma ilikuwa ni lazima kupata nguzo kutoka katika nchi za Afrika Kusini na Uganda, ambapo ilichukua muda wa miezi saba hadi mwaka mzima bila mwananchi kuunganishiwa umeme.
“Ni matumaini yetu kwamba nguzo ambazo zinazalishwa hapa sasa zitasaidia sana kupelekwa kwa haraka katika mikoa ya Kigoma, Geita, Kagera, Katavi na Shinyanga, alisema Waziri Kalemani, na kuongeza kuwa mameneja na wakandarasi wa mikoa hiyo hawatakuwa na kisingizio cha kutopeleka umeme kwa wananchi.
Waziri Kalemani amesema kuwepo kwa kiwanda hicho kutafanya bei ya nguzo katika mikoa hiyo kushuka hadi kufikia laki 240,000 ikilinganishwa na bei ya nguzo zilizokuwa zinatoka mkoani Njombe ambazo gharama yake ilifikia shilingi laki tatu.
Uzinduzi wa kiwanda hicho cha kuzalisha nguzo za umeme umeshuhudiwa pia na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, ambaye amesema serikali itaendelea kujenga vyuo vya ufundi stadi ili kuzalisha vijana wenye ujuzi wataotumia fursa za viwanda vinavyojengwa katika maeneo yao kupata ajira.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Qwihaya General Enterprises Co.Ltd, Leonard Mahenda, amesema kiwanda kimeweka mpango wa kuandaa miche bora ya miti ambayo itagawiwa kwa wananchi kwa ajili ya kupanda katika ekari 100 kila mwaka kuanzia mwaka kesho.
Wakati huo huo Mkurugenzi huyo wa kampuni ya Qwihaya, amemuadi Waziri wa Elimu Profesa Ndalichako, kuwa kampuni yake italipa gharama ya uwekaji umeme katika shule zote za msingi na sekondari zilizopo wilayani Kasulu.
Aidha kiwanda hicho kinatarajia kuajiri watu zaidi ya 100 ambao ni wakazi wa kata ya Heru Juu, ambapo baadhi ya wananchi wa kata hiyo, wakiwemo Festo Michael na Akida Bahisa, wamesema kiwanda hicho kimeongeza fursa kwao kwa kunufaika kupata ajira na kuuza miti yao kwa bei nzuri.