Na Munir Shemweta, WANMM IRINGA
Waziri wa Adhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuanza kujitathmini katika idadi ya hati za ardhi wanazotoa kwa wamiliki wa ardhi kwenye halmashauri zao.
Alisema Wizara yake itaanza kutangaza wilaya itakayoongoza katika Upangaji, Umilikishaji na Utoaji Hati za ardhi kwa wananchi ili kubaini hamashauri ambazo ziko nyuma katika kutoa hati za ardhi kwa wananchi.
Lukuvi alisema hayo jana katika mkutano wake wa kusikiliza na kutatua kero za ardhi kwa wananchi wa mkoa wa Iringa kupitia programu ya Funguka kwa Waziri uliyofanyika ukumbi wa Siasa ni Kilimo katika Manispaa ya Iringa,
‘’Mkurugenzi ajione fahari kuwaezesha wananchi kwa kupima na kuwapatia hati, kama Mkurugenzi huwezi kutoa hati miliki hata mia moja basi wewe hufai’’ alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Lukuvi, kumilikisha na kumpatia mwananchi hati ya ardhi ni kumuwezesha kiuchumi kwa kuwa anaweza kuitumia hati kwenye shughuli za kimaendeleo na kusisitiza kuwa wakurugenzi wa halmashauri wahakikishe wanapanga na kuwamilikisha maeneo wananchi.
Aidha, Lukuvi alisema kwa sasa wizara yake imejipanga kuhakikisha inasogeza huduma za ardhi karibu na wananchi kwa kuanzisha ofisi za mikoa zitakazokuwa na watendaji wote wa sekta ya ardhi kama vile Wapimaji, Wathamini, Wataalamu wa Mipango Miji pamoja na Wasajili.
‘’Sasa Wapimaji, Wathamini na Wapangaji watakuja hapa Iringa, muundo unaanza mwezi ujao lengo ni kuwapunguzia usumbufu wananchi katika kupata huduma za ardhi’’ alisema Lukuvi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, katika kuboresha huduma za sekta ya ardhi, Wizara yake itatumia mifumo unganishi itakayorahisisha utendaji kazi kwa wataalamu wa sekta ya ardhi ambapo kazi kubwa itakuwa ikifanyika kielektroniki badala ya kutumia makaratasi aliyoaeleza kuwa wakati mwingine husababisha tamaa kwa maafisa ardhi.
Alitolea mfano mkoa wa Dar es Salaama kuwa, ushaanza kutumia mfumo unganishi ambapo sasa wamiliki wa ardhi katika mkoa huo wanapatiwa hati za kielectroniki na kubainisha kuwa lengo la kuwa na mfumo unganishi ni kuondoa urasimu na kurahisisha utendaji kazi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Hapi alieleza kuwa mkoa wake umejitahidi kupunguza kero na migogoro ya ardhi iliyokuwepo miaka ya nyuma kwa kuanzisha utaratibu wa kuwafuata wananchi kwenye maeneo yao kupitia programu ya Iringa Mpya.
Alimueleza Waziri Lukuvi kuwa, kama angekuja mwaka mmoja na nusu uliopita basi ukumbi aliofanyia mkutano wa Funguka kwa Waziri ungekuwa umejaa wananchi wenye kero za ardhi lakini jitihada za mkoa wake zimesababisha mkutano huo kutokuwa na idadi kubwa ya wananchi wenye migogoro ya ardhi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
‘’Muda mwingi nautumia kwenda kwa wananchi na kazi za ardhi zina changamoto kubwa na njia pekee ya kukabiliana nazo ni kutenda haki bila kujali uwezo, kabila ama dini ya mtu’’ alisema Hapi.
Social Plugin