NA.MWANDISHI WETU
Maandalizi ya maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru yamefikia hatua za kuridhisha huku Serikali ikieleza kuwa sherehe hiyo itapambwa na onesho maalum la Jeshi la Jadi la sungusungu kutoka Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameeleza itakuwa ni mara ya kwanza kwa jeshi hilo kuonesha namna wanavyofanya kazi za ulinzi katika maeneo yao ili kuendelea kuenzi nia ya Rais wa Awamu ya Tano Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli ya kuilinda amani na utulivu uliopo nchini.
Waziri alieleza hayo mapema Novemba 30, 2019 alipotembelea na kukagua maandalzii ya onesho hilo yanayoendelea katika Kijiji cha Hunghumalwa Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.
“Hii itakuwa ni mara ya kwanza kuwa na onesho hili maalum ambalo linatukumbusha nia ya Mhe. Rais ya kuilinda amani iliyopo na kuhakikisha haichezewi kwa gharama yoyote na kuona namna tunavyojivunia jeshi hili lililoundwa katika misingi na maadili mema ya amani na utulivu,” alisema waziri Mhagama
Aliongezea kuwa, Jeshi hilo litajumuisha zaidi ya sungusungu 1300 watakaoshiriki kwa siku hiyo kwa kuongozwa na Manji wao pamoja na Mtemi wa Wilaya Mogan Shimbi.
Sambamba na hilo maandalizi mengine ikiwemo, uandaaji wa uwanja wa CCM Kilumba, mazoezi ya Majeshi (Gwaride), Usafi wa mazingira pamoja na vikundi vya burudani yanaendelea mkoani hapo.
“Maandalizi muhimu ikiwa ni pamoja na marekebisho ya miundombinu katika uwanja yanaendelea pamoja na maandalizi muhimu ikiwemo, kutoa mialiko, kuandaa malazi kwa wageni, kuandaa vikundi vya ngoma za asili, kuandaa gwaride , kuandaa wanafunzi wa watakaoumba umbo la bendera, pamoja na nyimbo za kizazi kipya na mahitaji mengine muhimu yapo katika hatua za kuridhisha,” alisema Waziri Mhagama
Aidha, kutakuwa na vikundi vya burudani ikiwemo; ngoma za asili kutoka mkoa wa Mara (Ritungu) na mkoa wa Mwanza, wimbo maalum kutoka Zanzibar pamoja na kwaya ya AIC Mwanza na bendi ya Tanzania One Theatre (T.O.T) vitatumbuiza.
Alifafanua kuwa maonyesho hayo yatakayofanyika Desemba 9 yatajumuisha gwaride maalumu la heshima lililoandaliwa na vikosi vya ulinzi na usalama nchini.
“Watoto 3200 kutoka shule za msingi na sekondari za mkoa wa Mwanza wataonesha umbo la bendera ya Taifa letu,” alisema Waziri Mhagama
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.John Mongella aliwasihi Watanzania kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kuendelea kuilinda amani iliyopo kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu pamoja na kuendelea kuwa na uzalendo na kufanya kazi kwa bidiii kwa ajili ya kujiletea maendeleo.
Pia, aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo na kuendelea kujiandaa kwa bidii, usanifu na ubunifu wa kipekee katika kuiadhimisha siku hiyo muhimu.
“Ninamshukuru sana Mhe. Rais kwa kuelekeza maadhimisho haya kufanyika mkoani kwetu, niiwaase wananchi wa Mwanza kuitumia heshima tuliyopewa kwa kujitokeza kwa wingi katika siku hiyo ili kuunga mkono jituhada za Mhe. Rais wetu,” Alisisitiza Mongella.
Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 58 ya Uhuru na Miaka 57 ya Jamhuri kwa mwaka huu (2019) kitaifa yatafanyika Mkoani Mwanza katika viwanja vya CCM Kilumba ambapo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli na kupambwa na kauli mbiu inayosema “Miaka 58 ya Uhuru na Miaka 57 ya Jamhuri; Uzalendo, Uwajibikaji na Ubunifu ni msingi wa Ujenzi wa Uchumi wa Tifa letu”.
Social Plugin