WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inatarajia kufungua kitengo cha tiba za mifupa na misuli katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mara Kwangwa mara hospitali hiyo itakapokamilika kujengwa.
Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa hospitali hiyo iliyopo Manispaa ya Musoma mkoani Mara, leo mchana (Jumamosi, Desemba 7, 2019), Waziri Mkuu amesema kitengo hicho kitakuwa cha pili kwa ukubwa kikifuatia cha MOI Muhimbili.
“Lengo la kufungua kitengo hiki kwenye hospitali hii ni kusogeza huduma karibu na wananchi hususan wa Kanda ya Ziwa ambao kwa sasa wanategemea huduma hizo kutoka hospitali ya Bugando, jijini Mwanza ambayo pia imezidiwa kutokana na udogo wa kitengo hicho kwenye hospitali hiyo,” amesema.
Amesema kuwa ujenzi wa hospitali ya Kwangwa ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano ambapo mbali na kutoa huduma za afya lakini pia hospitali hiyo itafungua fursa zaidi za kiuchumi kwa mkoa wa Mara.
Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliagiza kutolewa kwa shilingi bilioni 15 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo uliokwama kwa zaidi ya miaka 40 na ameridhishwa na ujenzi wake unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Bw. Adam Malima alisema hospitali hiyo inatarajiwa kuanza kutoa huduma ya mama na mtoto ifikapo Februari, mwakani baada ya kukamilika kwa jengo A (wing A) mapema mwakani.
Bw. Malima alisema kuwa huduma za rufaa za hospitali ya mkoa wa Mara zinatarajiwa kuanza kutolewa Mei, mwakani huku huduma za kibingwa zikitarajiwa kuanza kutolewa kabla ya mwisho wa mwaka 2020.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa baada ya Rais Magufuli kupokea ombi kutoka mkoa wa Mara kuhusu kusaidia mkwamo wa ujenzi huo, Serikali ilitoa fedha zote (sh. bilioni 15) kwa mara moja ili kukamilisha ujenzi huo.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu akiwa ameambatana na mkewe Mama Mary Majaliwa, ameiwakilisha Serikali kwenye mazishi ya kaka wa mke wa aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania, Mama Maria Nyerere katika kijiji cha Kinesi kilichopo wilayani Rorya, mkoani Mara.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, DESEMBA 7, 2019.
Social Plugin