WAZIRI NDALICHAKO AAGIZA WANAFUNZI CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM WALIOTOA TAMKO LA KUIPA SERIKALI MASAA 72 WACHUKULIWE HATUA


Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof.Joyce Ndalichako, amesema Serikali imesikitishwa mno na tamko la Serikali ya Wanafunzi Chuo ya Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO), la kutoa saa 72 kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu iwe imetoa fedha za mikopo ya wanafunzi wote ambao wamekaa chuoni tangu kifunguliwe bila fedha.

Waziri Ndalichako amesema tamko la DARUSO ni kinyume na kifungu cha 4.1 kifungu kidogo cha 30 cha sheria ndogo za Chuo Kikuu ambacho kinazuia Mwanafunzi kupanga maandamano au kupanga njia ambayo itatumika katika kufanya maandamano.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma jana, Profesa Ndalichako alisema tamko hilo limetolewa kinyume cha utaratibu wa kutoa malalamiko na utovu wa nidhamu wa kiwango cha juu, ambacho hakiwezi kuvumilika, hivyo ametoa saa 24 kwa UDSM, kuwachukulia hatua na apewe taarifa hatua iliyochukuliwa.

Alisema kwa mujibu wa taratibu, uongozi wa Daruso unapaswa kuwasiliana na Mshauri wa Wanafunzi, ambaye anachukua malalamiko yao na kuyapeleka kwa Makamu Mkuu wa chuo.

Lakini, taratibu hizo zote hazijafuatwa na uongozi wa chuo hicho kikongwe nchini haujui chochote kuhusu madai na malalamiko hayo. Aidha, alisema wanafunzi 45,000 wa mwaka wa kwanza, walipaswa kupewa mikopo, lakini serikali imeongeza idadi na kufikia 49,485, na Sh bilioni 172 zimetolewa kwa ajili yao na wameshapata mikopo wote waliokidhi vigezo.

Alisema jumla ya wanafunzi 128,697 wa elimu ya juu, wanatarajia kunufaika na mikopo mwaka huu, ambayo kiasi cha Sh bilioni 447 zimepangwa kwa mikopo, na hadi sasa Sh bilioni 202 sawa na asilimia 45 zimeshapelekwa HESLB.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post