Na Mwandishi Wetu Katavi
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ametoa pikipiki 15 kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka katika Kata za Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi na kusisitiza matumizi mazuri na yaliyokusudiwa ya pikipiki hizo.
Akizungumza katika halfa ya ugawaji pikipiki hizo Waziri Ummy Mwalimu amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii nchini kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazozikabili jamii ya Watanzania kwa kuhakikisha wanawasaidia kupata fursa za kujiwezesha kiuchumi.
Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Mhe. John Pombe Magufuli imejikita katika kuhakikisha inawasaidia wananchi kuondokana na umasikini kwa kuwezesha kupata mikopo isiyo na riba kutoka katika Halmashauri ikiwa imelenga kundi la wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
“Msizitumie pikipiki hizi kwa mambo yenu binafsi na msizifanye bodaboda za biashara kazitumieni kuwafikia wananchi na kuhakikisha mnatatua changamoto zao ili waweze kujiletea maendeleo yao”
Aidha Waziri Ummy amezitaka Halmashauri zote nchini kuendelea kutenga asilimia 10 za mapato ili kuwezesha vijana wanawake na watu wenye ulemavu na mikopo hiyo iwe yenye tija na itakayowezesha kujikwamua kiuchumi” alisema Waziri Ummy.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Tanganyika Bw. Dotto Kwigema amesema kuwa pikipiki hizi zitakuwa chachu katika utendaji wa kazi wa Maafisa maendeo ya jamii na zitasadia kufuatilia na kuhamasisha wananchi katika kushiriki shughuli za maendeleo na kusaidia kupambana na ukatili wa kijinsia hususan kutokomeza mimba na ndoa za utotoni.
Ameongeza kuwa kwa Kata tatu ambazo Maafisa Maendeleo ya Jamii wake hawajapata pikipiki Wilaya ya Tanganyika itatenga Bajeti kwa ajili ya kununua pikipiki hizo ili kukamilisha kwa Kata zote kuwa na pikipiki kwa ajili ya Maafisa hao.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Kata Kabungu Wilayani Tanganyika Bw. Othman ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano wa kujenga mazingira wezeshi kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii hasa wa Kata kwa kuhakikisha wanapata nyenzo za usafiri ili kuweza kuwafikia wananchi masikini.
Pia Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Kata ya Wilayani Tanganyika Bi. Rose Mfikwa amemuhakikishia Waziri kuwa watatumia pikipiki hizo kuhamasisha jamii ya wana- Katavi na Wanatanganyika katika kuondoka na mila zinye hitilifu za kuozesha watoto na kupambana na ndoa na mimba za utotoni mkoani humo.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wanawake UN Women wametoa jumla ya pikipiki 15 kwa mkoa wa Katavi ikiwa ni jitihada za kuwezesha upatikani wa usafiri kwa lengo la kuwafikia wananchi hasa wa vijijini.
MWISHO