Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Serikali imesema kuwa imekusudia kuimarisha utoshelevu wa chakula nchini, ili kuchangia utoshelevu wa chakula katika ukanda wa Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi zilizo Kusini mwa Afrika (SADC), na kuwa kinara wa soko la mchele katika Jumuiya za Kikanda.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo tarehe 16 Disemba 2019 wakati akizindua Mkakati wa Taifa wa Kuendeleza Zao la Mpunga Awamu ya Pili (NRDS II) hafla iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa St Gaspar Jijini Dodoma.
Ili kufikia azma hiyo, Waziri Hasunga amesema kuwa serikali imeweka kipaumbele katika malengo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora za mpunga ambazo zinastahimili ukame na kuhamasisha matumizi ya teknolojia bora za uzalishaji zitakazo himili mabadiliko ya tabia nchi na Kupunguza gharama za uzalishaji na kuweka mifumo bora ya udhibiti ili mchele wetu uweze kushindana kwa bei na ubora na michele inayotoka nje ya nchi.
Malengo mengine ni Kuimarisha mifumo ya uzalishaji na masoko hususani kwa wakulima wadogo ili kukifanya kilimo cha zao la mpunga kuwa endelevu na kuhudumia soko la ndani na nje ya nchi; na Kuongeza eneo la kulima zao la mpunga katika maeneo ya umwagiliaji na yanayotegemea mvua.
Pamoja na mikakati hiyo muhimu kabisa ya kuimarisha zao la mpunga Pia amesema kuwa serikali imekusudia kuimarisha na kuboresha miundombinu ya umwagiliaji na kuwajengea uwezo wakulima kuhusu usimamizi wa miundo mbinu hiyo.
Ili kufikia malengo hayo Waziri Hasunga amesema kuwa Wizara ya kilimo kwa kushirikiana na wadau wa zao la Mpunga nchini itahakikisha inasimamia inaongeza eneo la uzalishaji wa mpunga kutoka hekta milioni 1.1 za mwaka 2018 hadi hekta milioni 2.2 ifikapo mwaka 2030; Kuongeza tija ya uzalishaji wa mpunga kutoka wastani wa tani 2.2 kwa hekta hadi kufikia wastani wa tani 4.4 kwa hekta ifikapo mwaka 2030; Kuimarisha kilimo cha umwagiliaji na kuhamasisha teknolojia za umwagiliaji zinazotumia maji kwa ufanisi na Kuongeza thamani ya zao la mpunga kutoka asilimia 10 hadi kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka 2030 ikiwa ni pamoja na kupunguza upotevu kabla na baada ya mavuno.
Kadhalika kuimarisha mifumo ya masoko na kilimo biashara; Kuongeza upatikanaji wa mbegu bora za mpunga pamoja na kuimarisha mifumo ya mbegu; Kuongeza upatikanaji wa mbolea kwa kuanzisha Viwanda vya kuzalisha na kuchanganya mbolea nchini ikiwa ni pamoja na mifumo ya masoko na usambazaji; na Kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, kuongeza thamani na kuboresha mifumo ya masoko na upatikanaji wa mitaji.
Waziri Hasunga amnetumia mkutano huo kuyasihi makampuni ya kimataifa ya JICA, HELVETAS, IRRI, RIKOLTO, BRiTEN, AGRICOM na Wadau wengine kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza Mkakati huo ambao umeainisha viashiria chanya vya kuendeleza zao la mpunga; na hatimaye kuifanya nchi kuwa mzalishaji na soko kuu la mchele katika ukanda wa Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi zilizo Kusini mwa Afrika.
Alisema kuwa pamoja na kukamilika kwa utekelezaji wa awamu ya kwanza ya Mkakati wa Kuendeleza Zao la Mpunga (NRDS I) na kuonesha mafanikio makubwa, ni dhahiri kuwa bado kunahitajika kuongeza tija na uzalishaji zaidi. Hivyo hiyo ndio sababu iliyopelekea Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo kuandaa Mkakati wa Kuendeleza Zao la Mpunga Awamu ya Pili (National Rice Development Strategy Phase II - NRDS II) utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka kumi (10) kuanzia Mwaka 2019/20 hadi Mwaka 2029/30.
Lengo kuu la Mkakati huo ni kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga, kuimarisha usalama wa chakula na lishe, pato la wakulima na Taifa kwa ujumla ifikapo Mwaka 2030.
Ameongeza kuwa Uandaaji wa Mkakati huo ni matokeo ya Mkutano Mkuu wa Coaliation for African Rice Development (CARD) uliofanyika Jijini Tokyo, Japani Mwezi Oktoba, 2018 ambao ulikuwa na malengo makuu mawili ambayo ni kufanya tathmini ya utekelezaji wa CARD awamu ya kwanza kipindi cha mwaka 2008 hadi 2018 na kuona namna gani awamu ya pili ya Mkakati huo itakavyotekelezwa kwa kipindi cha Mwaka 2019 hadi 2030.
MWISHO