Timu ya taifa ya soka ya Urusi
Urusi imefungiwa miaka 4 kutojihusisha na mchezo wowote duniani, baada ya kupatikana na hatia ya kufanya udanganyifu kuhusu vipimo na maabara juu ya utengenezwaji na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu michezoni.
Taarifa ya Shirika la kupinga dawa za kuongeza nguvu michezoni 'World Anti-Doping Agency' (WADA) leo Desemba 9, 2019, imeeleza kuwa Urusi inatakiwa kusimamishwa na mashirikisho yote yanayosimamia michezo duniani ikiwemo FIFA kwa upande wa soka pamoja na Kamati ya kimataifa ya Olimpiki (IOC).
Kufungiwa huko ni wazi kuwa Urusi itakosa michuano mbalimbali mikubwa ndani ya miaka hiyo ikiwemo Olimpiki 2020, itakayofanyika jijini Tokyo Japan, pamoja na FIFA World Cup 2022 nchini Qatar.
Uamuzi huu umekuja ikiwa ni miaka minne imepita tangu uchunguzi mkali uanze kufanyika, ambapo tayari viongozi mbalimbali wa michezo nchini humo, wameshafungiwa kwa hatia hizo hizo za kuhusika kuruhusu wanamichezo kutumia dawa za kuongeza nguvu.
WADA wameweka wazi kuwa Urusi kupitia maabara zao za Moscow, waligoma kuchunguzwa na baadaye walipokubali walitoa taarifa feki na kisha kufuta baadhi ya taarifa ambazo zingeeleza ukweli juu ya suala hilo.
Kwa upande wa klabu ya Saint Petersburg ambayo inajiandaa na mchezo wake dhidi ya Man City kwenye ligi ya mabingwa Ulaya, wao wataendelea pamoja na timu ya taifa itacheza EURO 2020 kutokana na michuano yote hiyo kuandaliwa na UEFA na sio FIFA.
Hata hivyo wamepewa siku 21 kuweza kukata rufaa katika mahakama ya kimataifa ya michezo 'Court of Arbitration for Sport' (CAS).
Social Plugin