Na Adela Madyane - Malunde 1 blog Kahama
Watu wawili wamefariki dunia na wengine saba kujeruhiwa vibaya kutokana na ajali iliyohusisha basi la Napol Express kugongana uso kwa uso na Hiache katika eneo la Karagwa Kata ya Ntobo Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga.
Ajali hiyo imetokea baada ya gari aina ya Toyota Hiace yenye namba za usajili T 440 DHJ iliyokuwa ikielekea Kijiji cha Kakola Kata ya Bulyanhulu Halmashauri ya Msalala ambapo wakati Hiace ikikata kona majira ya usiku ilikutana na basi la Napol Express yenye namba za usajili T 155 CKG hali iliyopelekea kugongana uso kwa uso na kusababisha watu wawili kufariki dunia hapo hapo na wengine saba kujeruhiwa vibaya.
Aidha kwa mujibu wa vyanzo vyetu vinaeleza kuwa gari hiyo aina ya Toyota hiace kutokana na kutembea huku ikiwasha taa moja ndiyo chanzo cha kugongwa na basi ubavuni upande wa kulia na kwamba wakati ajali hiyo ikitokea basi lilikuwa ikitokea Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza kuelekea Wilayani Kahama.
Jummane Kisendi ni mwenyekiti wa kitongoji cha Kalagwa, Kata ya Ntobo Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama akizungumza na Malunde 1 blog alisema kuwa yeye ni shuhuda wa tukio hilo na hivyo baada ya tukio hilo alitoa taarifa na kuwapigia simu polisi na hospitali ya Halmashauri ya mji wa Kahama ili kutoa msaada zaidi na kuokoa maisha ya abilia hao.
Kaimu mganga mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kahama Dk. Antar Fereji akizungumza na waandishi wa Habari alisema kuwa Januari 20 mwaka huu majira ya saa mbili usiku walipokea miili ya watu wawili waliofariki dunia katika eneo la ajali na wengine 7 kujeruhiwa vibaya kutokana na ajali hiyo.
Dk. Antar Fereji aliwataja watu waliofariki dunia katika ajali hiyo kuwa ni Dephina Muluno (30) na Fundi Saidi (34) wote wakiwa wanawake, na kuongeza kuwa miili hiyo imekwisha tambuliwa na ndugu na imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwaajili ya taratibu zingine za mazishi.
Akizungumzia upande wa majeruhi alisema kuwa kati ya watu saba wanawake ni wanne waliojulikana kwa majina ya Lucia Ndala (7), Kulwa Hamisi (20), Zainabu Ramadhani (42), na Kalekwa Hangaiki(33) wote kutoka Kakola, huku wanaume wakiwa watatu Abdul Saidi (15) kutokea Arusha, Ramadhani Abas (20) kutokea Niyogo na Juma Enos (38) kutokea Busoka Halmashauri ya mji wa Kahama.
Dk Fereji alisema kuwa kutokana na wagonjwa kuwa na majeraha makubwa watahamishiwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando Mwanza kwa ajili ya matibabu zaidi ambapo watu watano ni pamoja na Kulwa Hamisi, Zainabu Ramadhan,Kalekwa Hangaiki, Ramadhan Hamisi na Juma Enos watasafirishwa.
Akizungumzua ajali hiyo, dereva wa Toyota hiace Juma Enos, ambaye pia ni miongoni mwa majeruhi alisema kuwa alipata ajali hiyo alipokuwa akipanda mlima katika eneo la kitongoji cha Kalagwa, alipokutana na basi ambalo lilikuwa mwendo kasi na kukiri ajali hiyo ilisababishwa na gari zote mbili kuwasha taa moja ambapo wote walihisiana kuwa ni boda boda na hivyo hiace kukwanguliwa upande wa ubavuni kulia na kusababisha ajali hiyo.
Akielezea mkasa huo zaidi dereva huyo alisema kuwa gari lake lilikuwa na taa moja ya upande wa kushoto na hivyo kumchanganya dereva wa basi aliyeamini mbele yake kuna pikipiki na sio gari.
Naye Abdala Saidi (15) mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari mwalimu Nyerere iliyoko Kata ya Segese ameeleza kwamba huenda ajali hiyo ikakatiza ndoto za masomo yake kwani alikuwa akitokea Jijini Arusha akielekea Segese kuanza Masomo yake ya kidato cha kwanza.
Muonekano wa Hiace baada ya ajali
Basu la Napol Express
Muonekano wa hiace upande wa pili
Muonekano wa Hiace baada ya ajali
Basu la Napol Express
Muonekano wa hiace upande wa pili
Social Plugin