Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Lugha Bashungwa (Mb) akizungumza jambo mara baada ya kutolewa Mafunzo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira iliyoandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na BRELA.
Na Robertha Makinda -Dodoma
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imetoa elimu ya Majukumu yao kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira katika ukumbi wa Bunge leo tarehe 18/01/2020.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na BRELA. Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uelewa kuhusiana na kazi na shughuli zinazofanywa na Wakala katika kutoa huduma kwa jamii bila kusahau changamoto mbalimbali zinazoikabili BRELA ili Kamati iweze kushauri.
Katika mawasilisho yaliyotolewa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Brela Bi. Roy Mhando alieleza shughuli mbalimbali zinazofanywa na wakala ambazo ni kusimamia Sheria ya Makampuni Sura ya 212, sheria ya majina ya biashara sura ya 213, sheria ya alama za biashara na huduma, Sheria ya Usajili wa Hataza, Sheria ya Leseni za Viwanda, Sheria ya Leseni za Biashara. Ameileza Kamati kuwa Wakala inafanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha inatimiza majukumu yake kwa ufasaha na kuwafikia wateja wake kwa kutoa elimu kwa njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Kanali mstaafu Masoud Ally Khamis (Mb) amempongeza Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala kwa kazi nzuri anayoifanya na kuitaka Wakala kuendelea kutoa Elimu ili wadau wa biashara wajue huduma mbalimbali wanazotoa hasa katika maeneo ya pembezoni ambapo wadau wa biashara hawajui umuhimu wa kurasimisha biashara zao pia hawana uelewa wa matumizi ya Tehama.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Lugha Bashungwa (Mb) amewashukuru Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kwa maoni na mawazo yao waliyoyatoa ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa ya kuongeza ufanisi kiutendaji katika kuwahudumia wananchi pia ametoa maelekezo kwa BRELA kuwa waweke mkakati wa mawasiliano wenye lengo la kutangaza huduma zinazotolewa na Wakala kupita vyombo mbalimbali vya habari hasa kupitia redio za kijamii.
Mbunge wa Sumve Mhe. Richard Ndasa ameipongeza BRELA katika suala zima la kuwahudumia wateja kwani wamewawezesha wananchi wengi kupata huduma kwa urahisi kwani hivyo ndivyo inavyotakiwa katika kufikia uchumi wa kati wa viwanda ifikapo mwaka 2025.
Mbunge wa Ndanda Mhe. Cecil Mwambe amewashauri BRELA wawemakini kwenye kazi za kila siku ili kuondoa malalamiko na changamoto wanazopata wateja hii itasaidia kuongeza idadi ya wateja na pato la Taifa kwa ujumla.
Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Hawa Mwaifunga ameiomba BRELA wafike katika wilaya na Mikoa mbalimbali hapa nchi kwani huko kuna wadau wengi wanaohitaji kujua faida za kurasimisha biashara zao.
Mbunge wa Monduli Julius Kalanga Laizer ameipongeza BRELA kwa kuandaa mfumo wao ambao wanaendelea kuuhuisha na akapendekeza ni vema taasisi zingine za biashara kuunganishwa pamoja.Pia, amewapongeza watumishi wa BRELA kupitia kitengo cha TEHAMA wanaotoa msaada kwa wateja katika matumizi ya mtandao wa BRELA kwani wamekuwa wakisaidia sana wananchi pale wanapopata changamoto.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. Kanali mstaafu Masoud Ally Khamis (Mb) alihitimisha kikao kwa kuwashukuru wajumbe wa kamati hiyo na kuwahimiza kuendelea kuishauri vema Serikali ili kuweza kufikia adhima ya Uchumi wa Kati unaongozwa na Viwanda ifikapo 2025.
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Lugha Bashungwa (Mb) akizungumza jambo mara baada ya kutolewa Mafunzo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira iliyoandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na BRELA. Lengo la mafunzo hayo ikiwa ni kuwajengea uelewa kuhusiana na kazi na shughuli zinazofanywa na Wakala katika kutoa huduma kwa jamii bila kusahau changamoto mbalimbali zinazoikabili BRELA ili Kamati iweze kushauri.Mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Bunge Januari 18 ,2020.
Mbunge wa Monduli Mhe. Julius Kalanga Laizer akifafanua jambo wakati wa Mafunzo hayo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira iliyoandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na BRELA
Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Hawa Mwaifunga akizungumza jambo huku akiiomba BRELA kufika katika Mikoa na Wilaya mbalimbali hapa nchini kuhakikisha Wadau wengi Wanajiunga na kurasimisha biashara zao.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Kanali mstaafu Masoud Ally Khamis (Mb) akihitimisha Mafunzo hayo huku akimpongeza Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala kwa kazi nzuri anayoifanya na kuitaka Wakala kuendelea kutoa Elimu ili wadau wa biashara wajue huduma mbalimbali wanazotoa hasa katika maeneo ya pembezoni ambapo wadau wa biashara hawajui umuhimu wa kurasimisha biashara zao pia hawana uelewa wa matumizi ya Tehama.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Brela Bi. Roy Mhando (aliyesimama) akitoa mawasilisho yake wakati wa Mafunzo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira iliyoandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na BRELA.
Mbunge wa Ndanda Mhe. Cecil Mwambe (kushoto) akitoa ushauri kwa BRELA kuhusiana na kuaondoa malalamiko na changamoto wanazozipata wateja wao kuhakikisha wanazifanyia kazi na hatimae kusaidia kuongeza Idadi ya wateja na pato la Taifa kwa ujumla ,kulia ni Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Hawa Mwaifunga
Baadhi ya Wafanyakazi wa BRELA wakiwa na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu
wa pili kutoka kushoto Kabla ya kuingia Kwenye semina ya Kamati ya Bunge Wizarani ya Viwanda, Biashara na Mazingira.Pichani kulia ni Mbunge wa Sumve Mhe. Richard Ndasa akiipongeza BRELA
katika suala zima la kuwahudumia wateja,huku Wananchi wengi wakiwezeshwa kupata huduma kwa urahisi,kushoto ni Mbunge wa jimbo la Igalula Mhe.Musa Ntimizi.
--
Social Plugin