Jengo la Bijampola lililoungana na vyumba vya kulala wageni
Na Mwandishi wetu
Imebainika kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi (CCM) Wilaya ya Kahama Sipilaus Bijampola anamiliki nyumba bubu ya kulala wageni maarufu kama Danguro huku nyumba hiyo ikitumiwa na wanawake kwa biashara haramu ya ngono.
Uwepo wa jengo hilo umebainika jana Januari 28,2020 wakati na mkuu wa Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga, Anamringi Macha alipofanya ziara ya kushtukiza ili kuhimiza suala la usafi katika nyumba mbalimbali za kulala wageni pamoja na kumbi za starehe.
Ziara hiyo ililenga kufanya ukaguzi katika vyumba mbalimbali wanakolala wanawake hao pamoja na kuzungumza nao ili kujua zaidi shughuli walizonazo ikiwa ni pamoja na kuwasisitiza kufanya usafi vyumbani mwao.
Akiendelea na zoezi la ukaguzi, Macha alishangazwa na kitendo cha vyumba katika nyumba ya kulala wageni inayomilikiwa na Sipilaus Bijampola iliyopo Kata ya Nyihogo Mjini Kahama kukithiri kwa uchafu huku vikitoa harufu mbaya.
"Mazingira niliyokuta hayakuwa rafiki na yanatia mashaka kuwa hilo ni Danguro,vyumba vinadaiwa kuwa ni Guest house ni vichafu,ukaaji wa mule ndani ya vyumba,haukuturidhisha, ulitutia mashaka kuwa ni sehemu panapofanyika biashara haramu,biashara za kihuni",amesema Macha.
DC Macha alieleza kukerwa na kitendo cha biashara haramu kama hiyo pamoja na uchafuzi wa mazingira kuendeshwa na kiongozi ngazi ya chama kinachoongoza Serikali, na kutumia fursa hiyo kuziagiza Mamlaka zinazohusika kutembelea nyumba hiyo ili kujiridhisha na uhalali wa Biashara hiyo pamoja na uchafu huo iwapo itabainika kuendeshwa kinyume na utaratibu wa serikali hatua za kisheria zichukuliwe.
“Kwa kweli ni kitendo cha ajabu sana kama biashara hii inafanyika na mamlaka zinazohusika zipo vyumba ni vichafu, Vinatoa harufu mbaya na binadamu wanaishi katika nyumba hii naagiza mamlaka zinazohusika wafike hapa kuchunguza ili kubaini ukweli lakini suala la usafi maafisa wapo, kama kuna ukiukwaji wa sheria hatua zichukuliwe,” amesema Macha.
"Nilimpigia simu mmiliki Sipilaus Bijampola na kumuonya nikimtaka azingatie sana suala la usafi ndani na nje ya nyumba hiyo inayosemekana kuwa ni Gesti bubu ili kuepuka maradhi yatokanayo na uchafu. na pia nilimuagiza Bwana Afya wa halmashauri ya Mji Kahama amwelekeze mmiliki wa nyumba hiyo afanye marekebisho",ameongeza.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama Anderson Msumba akizungumza jana na waandishi wa habari ofisini kwake alikiri Bijampola kubainika na makosa mbalimbali ya ukwepaji wa kodi ya Serikali likiwemo la uchafu na kuongeza kuwa hivi karibuni alipigwa faini na kulipa kiasi cha shilingi 800,000 kwa ajili ya uchafuzi wa mazingira.
“Kumbukumbu zangu zinaonyesha tulienda Umbwe gest house tulimpa leseni lakini tulipofanya ukaguzi baadaye tulikuta Danguro tukamfungia, tulipoendelea na ukaguzi huo tulienda Bijampola tukakuta naye anamiliki Danguro pia tukamfungia na kila ukaguzi tukibaini hayo tunachukua hatua ya kuwafungia,” amesema Anderson Msumba na kuongeza.
“Licha ya agizo la mkuu wa Wilaya kuzitaka mamlaka kufika katika maeneo hayo sisi kama Halmashauri tunaendelea na ukaguzi na kubaini wanaokiuka sheria, Bijampola anapaswa kufanya biashara zake kwa kufuata misingi ya sheria zilizopo na sisi Halmashauri tunaendelea kuzisimamia, Tulienda tukakuta pachafu na kukiuka sheria kwa mujibu wa leseni tukamsitisha na kumtoza faini na tutaendelea kufungia madanguro,”
Hata hivyo Mkurugenzi wa baa ya Bijampola na nyumba hiyo ya kulala wageni Sipilaus Bijampola akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu yake ya kiganjani akiwa mjini Shinyanga akiendelea na vikao alikiri mkuu wa Wilaya kufika katika eneo la biashara zake.
“Hayo ni mambo madogo madogo suala la Dangulo haliwezi kufuta biashara zangu na wala sibabaishwi na Waandishi wa Habari kama Benki ya NMB walipiga mnada lakini na bado mmiliki ni mimi, mimi sina cha kusema zaidi mwandishi wa Habari”,alisema
Licha ya nyumba hiyo ya kulala wageni kudaiwa kuwa inatumika kuendesha biashara haramu ya ngono, biashara hiyo imezidi kushamiri na kufanyika wazi wazi katika maeneo mengi ya wazi na yale yenye mkusanyiko mkubwa wa watu katika Halmashauri ya Mji wa Kahama licha ya mamlaka husika kukemea vitendo hivyo mara kwa mara.