Na Tito Mselem Dodoma,
Waziri Biteko ameagiza uongozi wa Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na Wizara ya Madini kuandaa maonesho ya madini kwa lengo la kuelimisha Umma kwa watu wa Morogoro na mikoa jirani juu ya Sheria, Kanuni na fursa zilizopo katika Sekta ya Madini.
Hayo yamebainishwa leo January 08, 2020 na Waziri wa Madini Doto Biteko, alipofanya kikao na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Sanare, kilichofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Madini, Mtumba jijini Dodoma.
“Nichukue fursa hii kuwaelekeza wataalamu wote wa Wizara ya Madini na Taasisi zake kuhakikisha wanashirikiana na Mkoa wa Morogoro kuzitangaza fursa zinazopatikana katika Sekta ya Madini Mkoani Morogoro kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo kuandaa maonesho yatakayopelekea kuelimika kwa wananchi wa Mkoa huo,” alisema Waziri Biteko.
Aidha, Waziri Biteko amesisitiza ushirikiano katika kusimamia Sekta ya Madini kati ya Wizara na Mkoa wa Morogoro na kumpongeza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Morogoro Emmanuel Shija kwa kazi nzuri anazozifanya katika ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Waziri Biteko amesema maendeleo ya Sekta ya Madini katika Mkoa wa Morogoro yatatokana na wachimbaji wenyewe, hivyo Wizara na Mkoa inapaswa kuwalinda na kuwalea wachimbaji na wadau wote wa madini mkoani humo.
Akizungumzia changamoto inayowakabili wananchi wa Morogoro Biteko alisema ni pamoja na uelewa mdogo walionao juu ya masuala yanayohusiana na Sekta ya Madini kuwa ni kikwazo katika kupelekea maendeleo Mkoani humo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, ameonesha kufurahishwa na kitendo cha Mkoa wa Morogoro kuonesha mafanikio makubwa katika makusanyo ya mapato ya serikali kutoka shilingi 811,714,294.12 kwa mwaka 2017/2018 mpaka kufikia 1,031,865,068.41 kwa mwaka 2018/2019.
“Madini ya Ujenzi, Vito na Dhahabu tukiyasimamia vizuri hakika yatatuingizia fedha nyingi watu wa Morogoro, hivyo nikuombe Mkuu wa Mkoa ukalifanyie kazi hilo, pia sisi kama Wizara ya Madini tutashirikana na Mkoa wa Morogoro kuhakikisha wawekezaji wanakuja kuwekeza katika Sekta ya Madini Mkoani Morogoro,” alisema Nyongo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Sanare, amemuomba Waziri kupatiwa ushirikiano katika kuitangaza Morogoro kuwa ni Mkoa wa Madini na sio kilimo peke yake.
Pia Sanare, amesema, Mkoa wa Morogoro unampango wa kufufua viwanda vya Ceramics vilivyokuwepo ili kuongeza matumizi ya madini ya viwandani yanayopatikana katika Mkoa huo kwa wingi na kuendeleza uhamasishaji wa uanzishwaji wa viwanda vipya vya Ceramics.
Wakati huo huo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Morogoro, Emmanuel Shija, amesema Mkoa wa Morogoro una Jumla ya leseni 3082 za wachimbaji wadogo kati yake ni leseni 250 tu ndizo zinafanya kazi ya uzalishaji, hivyo Ofisi ya Madini inaendelea na zoezi la kufuta leseni zote zenye makosa.
“Mwaka 2019 jumla ya leseni 223 zilifutwa na jumla ya hati za makosa kwa leseni 836 zimetolewa, leseni hizo ziko kwenye utaratibu wa kufutwa ndani ya mwaka huu wa fedha endapo wamiliki wa leseni hizo hawatarekebisha makosa yao kama Sheria inavyoelekeza,” alisema Shija.
Kikao hicho kilicholenga kujadili changamoto na maendeleo ya Sekta ya Madini kwa Mkoa wa Morogoro ikiwa ni pamoja na kuangalia fursa zilizopo katika Sekta ya Madini katika kuharakisha maendeleo ya mkoa huo, kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Madini na Taasisi zilizo chini ya Wizara akiwepo Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini Prof. Shukrani Manya, Mkurugenzi Taasisi ya Jiolojia na Utafiti Tanzania Dkta Musa Budeba, Kamishna wa Madini Mhandisi David Mulabwa, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Madini Edwin Egenge, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Madini Augustine Ollal na wengine.
Social Plugin