Wazee wa Kitongoji cha Lwanda agalo kijiji cha Bubombi kata ya Bukura wilayani Tarime mkoani Mara wakimpatia zawadi ya kondoo Mbunge wa Jimbo la Rorya Lameck Airo baada ya kufurahishwa na msaada wa mbunge.
Na mwandishi wetu ,Rorya
Wanafunzi wa Kitongoji cha Lwanda agalo Katika Kijiji cha Kirongwe kata ya Bukura wilayani Rorya mkoani Mara wanalazimika kutembea umbali wa km 22 ili kupata elimu katika shule ya msingi ya Kirongwe.
Baadhi yao wamemua kuepuka umbali na kutembea mwendo wa km 3 kwenda kusoma shule ya Kadem-Uhuru Bey iliyopo nchini Kenya,jambo ambalo limemladhimu Mbunge wa jimbo la Rorya Lameck Airo(CCM) kutoa mabati 74 na mifuko ya saruji 60 ili kujenga shule shikizi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kirongwe Samwel Okeyo wakiwa kwenye mkutano wa Kitongoji hicho alimweleza Mbunge kero kubwa ya ukosefu wa shule inayowatesa wanafunzi kutembea km 22 kwenda na kurudi jambo ambalo limechangia utoro na wengine kuacha shule kwasababu ya umbali.
Akisoma Risala mbele ya mbunge huyo katibu wa kamati ya shule Kaunda Obando alisema kuwa wananchi wamekuwa wakichangishana fedha ili kujenga shule ya msingi yapata miaka 28 tangu mwaka 1992 lakini ujenzi umeshindwa kukamilika.
‘’Mbunge tunakupongeza sana umekuwa ukitoa fedha zako mfukoni kusaidia wananchi uliwahi kutuchangia milioni moja lakini bado hatujamaliza tumejenga maboma 2 ya madarasa,lengo letu ni kuanzisha shule hapa ili watoto wetu wasiteseke’’alisema Obando.
Aliongeza kuwa sababu ya kutokamilika ni kutokana na mazingira ya kijiografia ,ugumu wa maisha kwa baadhi ya wananchi na kitongoji hicho hakina mapato ya fedha zaidi ya wananchi kuishi kwa kutegemea kilimo.
Diwani wa Kata ya Bukura Meshark Mamba(CCM) alisema kuwa viongozi wa awamu zilizopita walishindwa kukamilisha ujenzi kutokana na baadhi yao kula fedha za michango ya wananchi.
Mwanafunzi wa darasa la pili shule ya msingi Kirongwe Deus Bessy aliiambia Uhuru kuwa umbali mrefu unawakatisha tamaa watoto wenye umri mdogo.
‘’Tunatembea umbali mrefu tunachoka sana tukipata shule hapa itatusaidia hasa sisi watoto wadogo tunateseka wengine wanaamua kuacha shule maana shule iko mbali ndoto zangu ni kuwa mwalimu’’,alisema Bessy.
Mwanafunzi wa Darasa la tano Visent Okech alisema’’Shuleni unatakiwa kufika saa 1:30 unatoka saa 6 mchana kwenda nyumbani kupata chakula kwakuwa umbali ni mrefu tunalazimika kubaki shuleni tunashinda njaa mpaka saa 10 jioni tunatawanyika kurudi nyumbani”,alisema Okech.
Fedrik Salmu mkazi wa Kitongoji cha Lwanda agalo alisema kuwa usimamizi wa ujenzi ndiyo tatizo kwakuwa zimekuwa zikiwekwa bajeti na wananchi kuchangia fedha lakini fedha zinaliwa pasipo kufanya maendeleo na kusababisha majengo kubomoka.
Thomas Maucha aliwataka Viongozi kuwa makini na kusimamia fedha zinazotolewa pamoja na kuwasomea mapato na matumizi kwakile alichoeleza kuwa shughuli zinapofanyika hawasomewi mapato na matumizi ambazo ni fedha za wananchi zilizochangwa.
Mbunge Airo alisema kuwa ni vyema viongozi na wananchi kuungana kukamilisha ujenzi ili kuwanusuru watoto huku akitoa mabati 74 na kuahidi mifuko 50 ya saruji akiungwa mkono na Diwani wa kata ya Bumera Deogratus Ndege(CCM)aliyeahidi kutoa mifuko 10 ya Saruji.