Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HALMASHAURI UVINZA YAMKERA NAIBU WAZIRI MABULA

Na Munir Shemweta, WANMM UVINZA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameijia juu halmashauri ya wilaya ya Uvinza mkoa wa Kigoma kwa kushindwa kuihudumia idara ya ardhi na kusababisha watumishi wa idara hiyo kugharamia baadhi ya vifaa ili kutekeleza majukumu yao.

Hali hiyo ilibainika jana katika halmashauri hiyo wakati Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa kigoma.

Akiwa katika Masijala ya Ardhi ya halmashauri ya wilaya ya Uvinza, Dkt Mabula alibaini utunzaji majalada ya ardhi usiofuata taratibu huku baadhi ya hati zikiwa hazijakamilishwa kwa ajili ya kuwapatia wamiliki wa ardhi katika halmashauri hiyo tangu mwaka 2018.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwajia juu watumishi wa sekta ya ardhi katika halmashauri hiyo kwa kushindwa kutekeleza majukumu ipasavyo jambo alilolieleza kuwa linachangia uwepo migogoro ya ardhi sambamba na kuwanyima wananchi fursa ya kupata hati.

Dkt Mabula aliagiza hati zote ambazo taratibu zake zishakamilishwa ikiwemo wamiliki wake kusaini hati hizo kupelekwa Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Magharibi ndani ya wiki moja  kwa ajili ya kukamilishwa na kupatiwa waombaji.

Hata hivyo, baada ya kuwajia juu watumishi wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya Uvinza ndipo Afisa Ardhi wa halmashauri hiyo Manyama Makongo alipomueleza kuwa idara hiyo inashindwa kutekeleza majukumu yake kutokana na kukosa vifaa jambo lililosababisha kuamua kuchukua  ‘Printer’ yake binafsi na kuipeleka kwenye ofisi hiyo kwa ajili ya kusaidia kazi za idara.

Hali hiyo siyo tu ilimshutua na kumshangaza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi bali ilimsononesha kwa kuona watumishi wa sekta ya ardhi katika halmashauri hiyo wanatumia fedha zao za mifukoni kuendesha ofisi jambo alilolieleza kuwa halikubaliki.

‘’Hapa jitihada za ziada zinahitajika, halmashauri ipo inashindwa kuihudumia idara ya ardhi, halafu watumishi wanatumia fedha zao za mfukoni hili halikubaliki lazima niwasiliane na Waziri Jafo kuhusiana na suala hili’’ alisema Dkt Mabula.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mabula, idara za ardhi katika halmashauri nyingi nchini zimekuwa kama watoto wa kambo kutokana na wakurugenzi wa halmashauri kutozitengea bajeti ya kutosha jambo linalofanya idara kufanya kazi katika mazingira magumu.

Katika hatua nyingine Mkuu wa wilaya ya Mpanda mkoani Katavi Lilian Matinga na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Enelia Lutungulu wamewaokoa Maafisa Ardhi wa halmashauri hiyo wasitumbuliwe kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ikiwemo kutokamilisha utoaji wa hati za ardhi kwa muda mrefu.

Walionusurika ni Afisa Ardhi Mteule wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Spear Mwalukasa ambaye ilielezwa yuko katika mafunzo  na  Afisa Ardhi Ezekiel Bichuro. Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alisema kutokana na Maafisa hao kuzembea kukamilisha hati kwa muda mrefu basi hawafai kuendelea na nafasi zao kwa kuwa wanakwamisha utoaji hati ambao sasa unaweza kufanyika ndani ya mwezi mmoja pale taratibu zote zinapokuwa zimekamilika.

Hata hivyo, Mkuu wa wilaya ya Mpanda Lilian Matinga na Kaimu Mkurugenzi Enelia Lutungulu waliwatetea kwa kueleza kuwa maafisa hao hawana muda mrefu katika idara hiyo na makosa yanaweza kuwa yalifanywa maafisa waliopita.

Naibu Waziri Mabula alielekeza maafisa hao kupewa barua za onyo kwa kuwa muda wa miezi mitatu waliopo katika idara hiyo wangeweza kuonesha jitihada za kukamilisha hati na kuagiza hati zilizopo zikamilishwe katika kipindi cha mwezi mmoja.

‘’Ikifika tarehe 30 Januari 2020 hati ziwe zimeenda kwa wenyewe, haiwezekani mtu amesaini tangu 2015 halafu mpaka sasa hajapatiwa hati yake, wapo wazembe wachache  wanaochafua Wizara lazima wapewe warning. Alisema Naibu Waziri Mabula.

Naibu Waziri Mabula pia alitembelea wilaya ya Tanganyika ambapo alionesha kutoridhika na kasi ya ukusanyaji mapato yatokanayo na kodi ya pango la ardhi na kuagiza halmashauri ya wilaya ya Tanganyika kuongeza kasi katika makusanyo sambamba na kupanga, kupima na kumilikisha viwanja kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Afisa Ardhi wa halmashauri ya wilaya ya Tanganyika Penina Simon kiasi cha shilingi milioni 18,069,179.40 kilikusanywa hadi kufikia nusu ya mwaka wa fedha 2019/2020.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com