Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ITIGI KUKUSANYA SH BILIONI 20 MWAKA WA FEDHA 2020/21

Na Abby Nkungu, Itigi
HALMASHAURI ya Itigi katika wilaya ya Manyoni mkoani Singida inakusudia kukusanya na kupokea zaidi ya Sh bilioni 20.89 kutoka vyanzo vyake mbalimbali vya mapato kwa mwaka wa fedha 2020/21.


Akiwasilisha Mapendekezo ya Bajeti hiyo mbele ya Kikao maalum cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji John Mgalula, Ofisa Mipango Samwel Sendegeya alisema Sh bilioni 1.96 zitatokana na vyanzo vya mapato ya ndani wakati zaidi ya Sh bilioni 18.92 zitatokana na ruzuku ya Serikali Kuu na Wahisani.

Aidha, alieleza kuwa katika Mpango wa bajeti hiyo ya 2020/21, halmashauri itajikita zaidi katika kutatua changamoto mbalimbali za wananchi kwa kuongeza ukusanyaji mapato, kuwezesha wananchi kiuchumi, kuboresha mazingira ya kufanyia kazi watumishi, miundombinu ya shule na mazingira ya kujifunzia na kufundishia na kupunguza vifo vya wajawazito na watoto.

Pia, kuboresha huduma za afya kwa makundi maalum, kuimarisha huduma na upatikanaji dawa na vifaa tiba, kulinda vyanzo vya maji, kuondoa ujenzi wa makazi holela, kuboresha shughuli za ugani, ufugaji, usalama wa chakula, kuimarisha na kuendeleza uvuvi, kudhibiti wanyama waharibifu na uvamizi haramu maeneo ya hifadhi.

 Akijibu hoja kwa nini halmashauri imependekeza bajeti ijayo kuwa Shilingi bilioni 20.8 wakati lengo la bajeti inayoendelea (2019/2020) ya Shilingi bilioni 12.9 tu bado kufikiwa hata nusu yake, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Alli Minja alisema kupandisha bajeti ni namna bora zaidi ya kupandisha kiwango cha mapato ya halmashauri.

"Kumekuwa na ulegevu wa ukusanyaji mapato, hilo tutalifanyia kazi safari hii....tutafanikiwa na kufikia lengo. Matumizi yanaongezeka kila kukicha, hata mtoto huanza kunyonya, kunywa uji kisha kula ugali. Nasi hatuwezi kubakia hapo hapo. Hatuna namna, lazima tupandishe bajeti yetu" alifafanua.

Naye Mkurugenzi Mtendaji Bw Mgalula akijibu hoja ya Diwani wa Viti maalum, Rehema Chizumi juu ya uhaba mkubwa wa watumishi wa kike katika halmashauri hiyo, alisema njia bora ya kuweza kuwabakisha ni kuweka mazingira ya kazi na makazi katika hali ya kuvutia ili wasifikirie kuhamia sehemu nyingine.

"Lakini Mwenyekiti, mbinu nyingine nzuri ingawa sio rasmi ya kuwafanya watumishi hawa wa kike wanaokuja kwetu waendelee kubaki nasi ni wananchi waishio hapa, kuwaoa" alisema kwa mzaha Mkurugenzi huyo huku hoja hiyo ikiungwa mkono na idadi kubwa ya madiwani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com