Ni kwamba mnamo tarehe 21/12/2019 mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la MASUOD MUSA MOHAMED [47] mfanyabiashara na mkazi wa makambako mkoani Njombe aliletwa kwa gari ya wagonjwa [Ambulance] katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya akiwa anasumbuliwa na ugonjwa wa mapafu na mnamo tarehe 23/12/2019 majira ya 05: 00 alfajiri mtu huyo alifariki dunia na ndipo mmoja wa ndugu yake aitwaye HAMIS MUSSA HAMAD [61] mkazi wa Pambogo Iyela Jijini Mbeya aliuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka katika msikiti wa MASJID TAUFIQ uliopo Block Q Soweto kwa ajili ya kuoshwa na kuswaliwa ambapo baada ya shughuli hizo kukamilika mwili wa marehemu ulihifadhiwa kwenye jeneza lililokuwa msikitini hapo na kisha kusafirishwa kuelekea Makambako kwa mazishi ambapo siku hiyo hiyo majira ya saa 18:00 jioni ulizikwa.
Baada ya kumaliza mazishi jeneza hilo lilibaki kwenye msikiti wa Makambako baada ya kukosa usafiri wa kulirudisha Mbeya kwa siku hiyo.
Mnamo tarehe 31/12/2019 ALLY MOHAMED Mkazi wa Makambako alimkabidhi jeneza dereva wa lori ili aweze kulileta hapa Mbeya na kumpatia namba ya simu ya HAMIS MUSSA HAMAD ili alipokee jeneza hilo.
Aidha lori hilo lilikuwa limebeba mzigo wa nyanya ambapo baadhi zilikuwa zinashushwa soko la Soweto na zingine zinapelekwa Songwe, hivyo majira ya saa 01:00 usiku wa kuamkia tarehe 01.01.2020 dereva huyo alifika Soweto na kushusha nyanya pamoja na jeneza lakini alipompigia HAMIS MUSA HAMAD mtu ambaye aliyeambiwa kuwa atalipokea jeneza hilo hakuweza kupatikana hewani hivyo ilimlazimu dereva huyo kukaa mpaka saa 04:00 usiku wa tarehe 01.01.2020 bila mafanikio na ndipo aliamua kumuachia mmoja wapo wa walinzi wa sokoni hapa ili ikifika saa 05:00 alfajiri kipindi cha swala aweze kuwakabidhi jeneza msikitini hapo.
Sambamba na hilo alimuachia namba ya simu ya mpokeaji kwa ajili ya mawasiliano na kisha dereva aliondoka kwenda Songwe lakini mlinzi huyo alilitelekeza jeneza hilo pale liliposhushwa na kuondoka zake hali iliyosababisha taharuki kwa wafanyabiashara wa soko hilo pamoja na wakazi wa eneo hilo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, limefuatilia kwa karibu suala hili na nitumie nafasi hii kukanusha habari zilizokuwa zimeenea kwenye baadhi ya vyombo vya habari na mitando ya kijamii kwani uhalisia wa suala hilo ni huu, hivyo niwatake wafanyabiashara na wananchi wa mkoa wa Mbeya kuendelea na kazi/biashara zao kama kawaida.
Social Plugin