Tukio la mwanamke aliyekutwa kaburini
Wananchi wa Mtaa wa Fadhili Bucha Kata ya Buhalahala Halmashauri ya Mji wa Geita, wamekumbwa na taharuki, baada ya kumkamata mwanamke mmoja, Mariam Kaijage akichimba mchanga na kuchuma majani yaliyoota juu ya Kaburi walilozika mmoja wa wanafamilia wa mtaa huo.
Kaburi la Mwanafamilia aliyejulikana kwa jina la Abel Njige aliyezikwa Desemba 24, 2015 ndilo ambalo limechimbwa mchanga na mwanamke huyo kama ilivyoelezwa na mdogo wa marehemu.
Amesema kuwa kifo cha ndugu yake kilitokea ghafla siku chache baada ya kupatwa na maradhi ya akili, akiwa na hofu huenda anayetafutwa hivi sasa ni yeye.
Akiongea na waandishi wa habari katika eneo la tukio, mtuhumiwa huyo ambaye awali alishikiliwa katika ofisi ya mtaa wa Fadhili Bucha kwa mahojiano zaidi kabla ya kuachiwa huru amesema mchanga huo ulikuwa ni tiba ya mwanaye anayesumbuliwa na maradhi ya miguu kwa muda mrefu.
Hata hivyo Doto anashangazwa na uongozi wa mtaa huo kumwachia huru mwanamke huyo kabla hajaeleza kwa kina lengo la yeye kufanya hivyo.
Pamoja na uongozi wa mtaa huo kugoma kuzungumzia sakata hilo, Mwenyekiti wa chama cha Waganga wa Tiba Asili Tanzania (CHAWAWATA) akatoa wito kwa jamii kuwaepuka waganga matapeli, huku Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjori Mwabulambo akielezea hatua walizochukua kudhibiti ramli chonganishi zinazopelekea mauaji ya watu mbalimbali wakiwemo vikongwe pamoja na albino.
Chanzo - EATV