Veronica Kazimoto na Rachel Mkundai
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, amewahimiza watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi, na kwa kuzingata misingi wa Sheria za kodi ili kuhakikisha kuwa TRA inaendelea kuvunja rekodi ya makusanyo ya mapato kama ilivyokuwa katika mwezi Septemba na Desemba, 2019.
Pia, amewapongeza watumishi wote wa Mamlaka hiyo kwa kujituma na kupelekea Serikali kukusanya mapato kiasi cha Sh. trilioni 9.341 sawa na ufanisi wa asilimia 47.67 ya lengo la kukusanya sh. trilioni 19.595 kwa mwaka wa fedha 2019/2020 katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2019/2020 yaani kuanzia Julai hadi Desemba 2019.
Akizungumza wakati wa mkutano wa mapitio na tathmini ya utendaji kazi wa nusu mwaka 2019/20 wa Mamlaka hiyo uliofanyika hivi karibuni jijini Arusha, Bw. James alieleza kuwa, mapato makubwa yanayotegemewa na Serikali ni makusanyo ya kodi ambapo aliwaasa watumishi wa TRA kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuongeza mapato na hatimaye Serikali iweze kutekeleza mipango yake iliyojipangia ya kuwaletea wananchi wake maendeleo.
“Ukiangalia mchanganuo wa makusanyo yote ya Serikali, sehemu kubwa sana ni kodi inayokusanywa na TRA. Kwa msingi huu, TRA inapofanikiwa kukusanya kodi kwa ufanisi mkubwa ndiyo mafanikio ya Serikali katika kutekeleza bajeti inayokuwa imepangwa kwa kipindi hicho,” alisema Katibu Mkuu huyo.
Aidha, aliwashukuru wananchi na walipakodi wote kwa kuendelea kulipa kodi kwa hiari na wakati ambapo makusanyo ya mwezi Septemba na Desemba, 2019 ni ishara kwamba, walipakodi kwa ujumla wao, wanaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuongeza mapato ya ndani na pia wameendelea kutambua umuhimu wa kulipa kodi baada ya kuona utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini inayofanywa na Serikali yao.
“Tunawashukuru sana walipakodi wa nchi hii kwa kutekeleza wajibu wao wa kisheria wa kuisadia Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania kukusanya kodi hiyo kubwa tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo. Kitendo hiki kiendelee na ikiwezekana iwe zaidi ya hapo”, alieleza Bw. James.
Akizungumzia suala la mifumo ya kieletroniki ya ukusanyaji mapato, ukiwemo mfumo wa mnada wa forodha kwa njia ya mtandao, Katibu Mkuu huyo, ameipongeza TRA kwa kuendelea kuboresha mifumo hiyo ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza mapato ya Serikali.
“Mfumo wa mnada wa forodha kwa njia ya mtandao ni mfumo mmojawapo kati ya mifumo mingi inayotumiwa na TRA katika kukusanya mapato. Mfumo huu, ambao umejengwa na Watalaam wetu wa TRA, umeonesha mafanikio makubwa kwa sababu unashirikisha watu wengi na kuleta ushindani wa haki kwa wote.
“Ni matarajio yetu kuwa, Serikali itapata mapato yake stahiki kutokana na kuuzwa kwa bidhaa zilizokaa muda mrefu bandarini tofauti na matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Ushuru wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004 na ni matumaini yetu kwamba, kuuzwa kwa wakati kwa bidhaa hizo kupitia mfumo huu, kutapunguza mrundikano wa bidhaa bandari na hivyo kuongeza ufanisi wa bandari zetu na vituo vingine vya forodha”, alieleza.
Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James amewaagiza viongozi wa TRA kufanya maboresho ya mifumo ndani ya Mamlaka hiyo mara moja pale watakapobaini mapungufu yoyote ambayo yanaweza kukwamisha utendaji kazi wa mfumo husika.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA, Dkt. Edwin Mhede, alisema kwamba, mkutano huo wa mapitio na tathmini ya nusu mwaka ulilenga kufanya maboresho katika utendaji kazi ili kuhakikisha kuwa malengo waliyopangiwa na Serikali yanafikiwa.
Dkt. Mhede aliongeza kuwa, TRA imepewa agizo na Serikali la kukusanya kiasi cha sh. trilioni 19.5 katika mwaka huu wa fedha 2019/20 ambapo pamoja na kufanya vizuri katika miezi ya Septemba na Desemba, 2019, alikiri kuwa bado Mamlaka hiyo haijafikia malengo ya makusanyo kwa asilimia 100. Hivyo, mkutano huo ulilenga kufanya marejeo na maboresho ya mikakati ya utendaji kazi itakayowezesha kufikia malengo hayo kwa asilimia 100.
“Kupitia Sheria ya Bajeti, SURA 439, TRA tumepewa agizo na Serikali la kukusanya mapato kiasi cha sh. trilioni 19.595 hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2020 na wakati tukitekeleza robo ya kwanza na ya pili ya mwaka wa fedha 2019/2020, hatukufanikiwa kufikisha asilimia 100 ya makusanyo ya robo hizo. Hii ndiyo moja ya sababu tumeona tukutane ili tubaini maeneo yenye mapungufu na kisha tufanye marejeo shirikishi ili tujisahihishe na kuweka mikakati itakayotuwezesha kufikia lengo”, alisema Dkt. Mhede.
Mkutano wa mapitio na tathmini ya utendaji kazi wa nusu mwaka 2019/20 wa TRA ulihudhuriwa na jumla ya washiriki 361 ukihusisha Menejimenti nzima ya Mamlaka, Mameneja wote wa Mikoa na Wilaya kutoka Tanzania Bara na Visiwani pamoja na baadhi ya watumishi wa Mamlaka hiyo.
Washiriki wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na wawakilishi kutoka baadhi ya Asasi za Serikali kama vile Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), Ofisi ya Rais - Tume ya Utumishi wa Umma, Ofisi ya Mganga Mkuu - Mkoa wa Arusha, na Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TAeSA) iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi na Ajira) ambapo kwa siku ya kwanza wawakilishi wa Asasi hizo walitoa maada kuhusu masuala mbalimbali ya kuisaidia TRA kuongeza makusanyo ya Serikali.
MWISHO.
Social Plugin