Macho Yote ya Watanzania leo ni Kwa Mbwana Samatta wakati atakaposhuka dimbani majira ya saa 4:45 usiku kuichezea timu yake mpya ya Aston Villa kwa mara ya kwanza, kwenye mechi ya Kombe la Ligi dhidi ya Leicester City katika Uwanja wa Villa Park.
Samatta alianza kujifua na wachezaji wenzake kwa mara ya kwanza Ijumaa iliyopita na Kocha wa Aston Villa, Dean Smith, alisema anaweza kuwa tayari kwa mchezo wa nusu fainali ya pili ya Kombe la Ligi (Carabao Cup) dhidi ya Leicester City leo.
Hata hivyo, mashabiki wa Aston Villa wametakiwa kuwa watulivu kwa Samatta kwa kuwa haitakuwa rahisi kwake kuzoea ‘ligi hiyo ngumu zaidi duniani’.
Samatta, 27, ambaye alikamilisha uhamisho wake kutoka KRC Genk ya Ubelgiji kwenda Villa wiki iliyopita kwa takriban pauni milioni 8.5 hadi anaondoka alishacheka na nyavu mara 10 kwenye mashindano yote huku msimu uliopita akiifungia timu hiyo ya jumla ya mabao 42.
Social Plugin