MBUNGE WA RORYA LAMECK AIRO ASHANGAA MILIONI 60 KUJENGA MADARASA MAWILI


Jengo la madarasa mawili,ofisi moja shule shikizi ya Mtakuja Kijiji cha Bubombi kata ya Bukura wilayani Rorya mkoani Mara ambalo ujenzi wake umegharimu milioni 60 fedha zilizotolewa kwa ufadhili wa Shirika EQUIP.
Mbunge wa Jimbo la Rorya Lameck Airo akizungumza jambo na Abas Amir ambaye ni Mganga mfawidhi wa Zahanati ya Bubombi Kata ya Bukura wakati wa ziara yake 
***
Na Mwandishi wetu,Rorya
Mbunge wa Jimbo la Rorya mkoani Mara Lameck Airo amezitaka Serikali za Vijiji kusimamia vyema fedha za wafadhili zinazotolewa kujenga miradi ya maendeleo.

Mbunge Airo alisema kuwa kuna baadhi ya miradi iliyojengwa haiendani na matumizi halisi ya fedha zitolewazo ukiwemo ujenzi wa shule shikizi ya Mtakuja Kijiji Cha Bubombi kata ya Bukura.

Shule hiyo imejengwa kwa sh.Milioni 60 kwa ufadhili wa EQUIP ambapo fedha zake ziliwekwa kwenye akaunti ya shule ya msingi Bubombi Kata ya Bukura ambayo ujenzi wake ulianza january 2019.

Airo aliyasema hayo mbele ya Viongozi wa Serikali ya kijiji cha Bubombi baada ya kusomewa taarifa ya matumzi ya milioni 60 ya ujenzi wa shule shikizi ya Mtakuja ambapo alishangaa kusikia kuwa kiasi hicho kimejenga madarasa mawili pekee,ofisi moja na choo chenye matundu 6 huku bado wakihitaji pesa nyingine milioni 6,620,000 kukamilisha ujenzi.

Akisoma taarifa ya ujenzi wa shule shikizi katibu wa kamati ya ujenzi wa shule hiyo ambaye pia ni mkuu wa shule ya msingi ya Bubombi Nelson Ryaga alisema kuwa mradi wa ujenzi ulianza 2019 kwa kujenga madarasa mawili ,ofisi moja,vyoo vya wanafunzi matundu manne na vyoo vya walimu matundu mawili ujenzi uliofadhiliwa na shirika la EQUIP kwa kutoa milioni 60.

“Ujenzi wa madarasa, ofisi na vyoo umekamilika ila kuna mapungufu yaliyojitokeza ya kutonunuliwa vifaa kama matenki mawili ya maji yenye thamani ya shilingi 600,000/=,Water gutters 600,000/=/=,Madawati 20 ya thamani 500,000/=,saruji mifuko 10 sawa na 200,000/=",alisema

Rangi lita 60 sawa na 120,000 jumla ikiwa shilingi 2,020,000 pamoja na shilingi 4,600,000 ambazo shule inadaiwa baada ya kukopa vifaa kwa mzabuni jumla ya fedha zote pungufu ni shilingi  6,620,000”,aliongeza Ryaga.

Ryaga alisema kuwa sababu kubwa ya upungufu unatokana na hali ya Kijiografia ya eneo iliyosababisha gharama kubwa ya ujenzi wa msingi ikilinganishwa na maelekezo ya B.O.Q,paa ya nyumba kufanyiwa marekebisho katika upauaji tofauti na B.O.Q pamoja na kutopatikana kwa mchango wa jamii kushiriki kuchangia nguvu kazi.

Mbunge Airo alisema hajaridhishwa na taarifa hiyo

"milioni 60 kujenga madarasa mawili !nawakati shule zingine tumejenga darasa moja kwa sh.milioni 15 na linakamilika kila kitu hizo pesa ni nyingi zilipaswa kubaki kiasi kingine au mngeongeza darasa lingine”,alisema Airo.

"Tena bado mnasema mmepungukiwa zaidi ya milioni 4 kukamilisha ujenzi, jamani viongozi wa Serikali ya vijiji simamieni fedha zimeletwa kwenye akaunti ya shule mnashindwaje kumsimamia mzabuni?kuweni makini na watu wa halmashauri na wahandisi unaambiwa kanunua vifaa kwa mtu fulani bati unauziwa 35,000 na wakati hilo hilo kwingine linauzwa 25,000-28,000

 Diwani wewe ndiyo Mwenyekiti WDC unashindwaje kusimamia fedha mpaka mnaingizwa mkenge?”alihoji Airo.

Diwani wa kata ya Bukura Meshack Mamba alisema ujenzi huo umefanywa bila Halmashauri kumshirikisha. 

"Ni kweli milioni 60 haziendani na huu ujenzi halmashauri ilileta mainjinia na mzabuni sisi hatukuwa na nguvu hatukuhusishwa kwenye shughuli ilikuwa inasimamiwa na wilaya na mkoa’’,alisema Mamba.

Diwani huyo anaongeza kuwa ujenzi huo ukikamilika na shule kuanzishwa itasaidia kupunguza umbali wa km.8 kwenda kusoma Bubombi na shule ya msingi Masonga itapunguza mrundikano shule ya Bubombi yenye wanafunzi 1090 kati ya hao wavulana wakiwa 550 na wasichana 540 na walimu 12, wanaume 8 na wanawake 4,idadi iliyosababisha kujengwa shule shikizi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post