Na Amiri Kilagalila-Njombe
Makamu mwenyekiti wa CCM Tanzania bara Mh.Philip Mangula amewakumbusha wanachama wa chama hicho nchini,marufuku iliyopo kwenye katiba kwa mwanachama yeyote anayetarajia kugombea au wakala wake kutoa misaada mbali mbali wakati uchaguzi unapokaribia.
Philip Mangula ametoa marufuku hiyo mkoani Njombe wakati wa kikao cha halmashauri kuu ya chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Njombe kilichofanyika katika ukumbi uliopo katika ofisi za chama cha mapinduzi mkoa wa Njombe zilizopo mjini Njombe.
Amesema kwa mujibu wa vifungu na kanuni zilizopo kwenye katiba ya chama zinaeleza wazi utaratibu na marufuku ya utoaji wa zawadi kwa wanaotarajia kugombea au mawakala kutoa misaada mbali mbali wakati uchaguzi unapokaribia kwa kuwa misaada hiyo huwa na lengo la kuvutia kura.
“Kanuni kifungu cha 6 kinasema ni marufuku kwa mwanachama yeyote anayetarajia kugombea au wakala wake kutoa misaada mbali mbali wakati uchaguzi unapokaribia,ambao ni dhahiri lengo lake ni kuvutia kura,isipokuwa kanuni hii haijamhusu Rais,mbunge mwakilishi au diwani ambaye yuko madarakani wakati huo kwa kuwa yeye atakuwa bado anao wajibu wa kuhudumia eneo lake la uongozi”alisema Mangula katiba inaeleza
Awali kabla ya kumkaribisha mwenyekiti wa CCM Tanzania bara,mwenyekiti wa chama cha mapinduzi mkoa wa Njombe Jasel Mwamwala,amewashukuru viongozi wa chama na serikali kwa kusimamia utekelezaji mzuri wa ilani ya chama cha mapinduzi na kuwaletea maendeleo wananchi,pamoja na kuiomba serikali kabla ya kufika uchaguzi wa Rais kukamilisha ujenzi mkubwa wa barabara za lami zilizoanza kujengwa mkoani humo.
“Tunaomba hizi barabara zikamilike ili tunapofika mwezi wa kumchagua Rais bara bara hizi zote ziwe zimekamilka na zinapitika kwasababu ndio ahadi na wananchi wanapohoji hivi kweli hizi barabara zitakamilika?sisi tunasema zitakamilika”alisema Jasel Mwamwala
Naye katibu wa chama hicho mkoa wa Njombe Ndugu Paza Mwamlima amesema kwa sasa mkoa wa Njombe unaendelea vizuri hususani kuelekea hatua za mwanzo za uchaguzi mkuu kwa kuwa katika zoezi la maboresho na kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura,chama hicho kimeweza kuhamasisha wanachama wake na kupelekea taarifa za awali kuonyesha wilaya ya Njombe kuandikisha wapiga kura 85,508 wilaya ya Wanging’ombe wanachama 24,450 wilaya ya Ludewa 14,936 na wilaya ya Makete 14,623.
Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho akiwemo katibu wa siasa na uenezi mkoa wa Njombe Erasto Ngole ametoa wito kwa wanachama wasipite kwenye kata na majimbo ya watu kuonyesha nia ya kugombea kabla chama hakijatoa maelekezo huku.Huku Anaupendo Gombela diwani wa kata ya Mdandu wilayani Wanging’ombe,ametoa wito kwa wanachama kuwaacha madiwani na wabunge wao huru kwa sasa ili watekeleze wajibu wao kabla ya mabalaza au bunge kuvunjwa.