Kamanda wa polisi Mkoa wa Kagera ACP Revocatus Malimi
Na Ashura Jumapili- Malunde 1 blog
Jeshi la Polisi Mkoani Kagera linaendelea na upelelezi wa matukio mawili yaliyotokea katika sehemu mbili tofauti na kusababisha vifo vya watu watatu akiwemo mtoto wa miaka miwili aliyeuawa kikatili baada ya kujisaidia haja kubwa kitandani.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Kagera ACP Revocatus Malimi,alithibitisha kutokea kwa matukio hayo jana January 16 mwaka huu wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake.
Malimi alisema tukio la kwanza limetokea wilaya ya Ngara maeneo ya Rubanda ‘A’Kijiji cha Kazingati Kata ya Keza tarafa Rulenge January 14 mwaka huu majira ya saa 12:00 jioni ambapo mtoto Bahati Juma miaka (02) Mshubi alifariki akiwa njiani wakati akipelekwa hospitali kupatiwa matibabu.
Alisema marehemu alikuwa na majeraha ya kuchomwa na moto sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo maeneo ya usoni,makalio na majeraha sehemu ya haja kubwa kwa kuchomwa kitu chenye ncha kali na mtuhumiwa ambaye ni baba yake mzazi.
"Desemba 27, 2019 usiku marehemu alikuwa akiishi na baba yake na mama yake wa kambo aitwaye Emiliana Juma miaka (28 )mwenye Asili ya Burundi baada ya mama yake mzazi kutalikiana na baba yake ambaye ni mtuhumiwa.
"Mama yake alimtelekeza mtoto kwa baba yake aliyeamua kuoa mwanamke mwingine, wakiwa wamelala kitanda kimoja na baba yake marehemu alijisaidia haja kubwa kitandani kitendo ambacho kilimkera baba na kuanza kumuadhibu vikali kwa kumfanyia ukatili huo na hakupelekwa hospitalini",alieleza Kamanda Malimi.
Alisema walianza kumtibu kwa njia za kienyeji hapo nyumbani baada ya kuona hali mtoto inabadilika na kuwa mbaya ,mtuhumiwa aliamua kutoroka nyumbani na kuanza kujificha kusikojulikana hadi majirani walipofichua tukio hilo kwa kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji na baadae kituo cha polisi January 14 mwaka huu
"Kwa ushirikiano wa wananchi na polisi tulifanikiwa kumkamata mtuhumiwa na anaendelea kuhojiwa na atafikishwa mahakamani",aliongeza.
Kamanda Malimi alisema tukio la pili jeshi hilo linawashikilia watu saba wanaotuhumiwa kuhusika kufanya mauaji ya ukatili kwa wanandoa wilayani Biharanulo mkoani humo baada ya kuwavamia na kuwakata kata na kitu chenye makali na kupelekea mauti.
Malimi alisema tukio hilo lilitokea huko katika Kitongoji cha Mangasini Kijiji cha Mabale Kata Nyakahura Tarafa ya Rusahunga wilaya Biharamulo January 14 mwaka huu majira ya saa saba usiku.
Alisema watu wawili wanandoa Elizeus Rubanie msubi miaka (35 ) na Juliana Joseph Mnyambo miaka (28) wote wakazi wa Manganisi tarafa ya Nyakahura ,wakiwa wamelala ndani ya nyumba yao walivamiwa na kuuawa kwa kukatwa kwa kitu chenye makali maeneo mbalimbali ya miili yao na watu ambao hawakufahamika.
Alisema imefahamika kuwa kabla ya tukio hilo kulikuwa na mgogoro wa ardhi kati ya marehemu Elizeus Rubanie na baadhi ya wana ukoo kwa muda mrefu.
Alisema eneo alilokuwa anaishi marehemu na familia yake aliachiwa na Babu yake mzaa baba ambaye aliwahi kuishi kijiji hicho kabla ya kuhama kwa shinikizo la wanajamii wakimtuhumu kuwa ni mwizi akaondoka na kumuacha mjukuu wake ambaye ni marehemu akiishi na familia yake.
Alisema baada ya Babu yake kuhama ,jamii wakiungana na baadhi ya wanandugu kwenye ukoo hasa mashangazi wake na marehemu wawili walianza kumsakama marehemu na familia yake kwa kumtolea vitisho vya kumdhuru maisha wakimtaka ahamae kwenye shamba hilo sababu hana haki ya kumliki ardhi hiyo.
Alisema mgogoro huo umekuwa ukisuruhishwa kwa muda mrefu na viongozi wa serikali ya kijiji.
Alisema siku ya tukio usiku marehemu akiwa amelala ndani na familia yake watu ambao hawakufahamika kwa idadi sura wala majina yao walivamia nyumba hiyo na kuwaua wanandoa hao kwa kuwakata kata sehemu mbalimbali za miili yao hadi wakapoteza maisha hapo hapo.
Alisema katika tukio hilo wanashikiliwa watu saba ambao ni Sophia Joseph miaka (45 ),Joseph Magambo (47 ),Alphonce Karoli (37 ),Marthine Makabe (36 )Alex Leopord (44) Salvatory Mwiliza (44 )na Aloyce Leopord (45 ).
Alisema uchunguzi unaendelea kuwabaini wengine watakaokuwa wanahusika na tuhuma hizo.
Social Plugin