Na Salvatory Ntandu - Malunde 1 blog
Mkazi wa kijiji cha Ninga wilayani Bukombe mkoani Geita Emmanuel Joseph (47) amehukumiwa kwenda jela miaka miwili au kulipa faini ya shilingi laki mbili na nusu na Mahakama ya wilaya ya Kahama baada ya kupatikana na hatia kwa makosa ya kuingia hifadhini bila kibali na kuchimba mchanga unaodhaniwa kuwa na dhahabu.
Akisoma hukumu hiyo leo Hakimu mkazi wa mfawidhi wa Mahakama hiyo Evodia Kyaruzi alisema kuwa Mahakama imemtia hatiani, Emmanuel baada ya kukiri mashitaka mawili yaliyokuwa yakimkabili Mahakamani hapo.
Kyaruzi alisema Emanuel katika shitaka la kwanza la kuingia katika pori la akiba kigosi moyowosi bila ya kuwa na kibali kutoka kwa mkurugenzi wa idara ya wanyamapori atatumikia kifungo jela mwaka mmoja au kulipa faini ya shilingi laki mmoja.
Katika shitaka la pili la kuchimba mchanga katika pori hilo la akiba atatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini ya shilingi laki mmoja na nusu ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine kwenye jamii wenye tabia ya kutenda makosa kama hayo.
Awali akisoma shauri hilo la jina namba 39 la mwaka huu mwendesha mashitaka wa Idara ya Wanyamapori Pachal Rwegoya alisema kuwa Emmaanuel alitenda makosa hayo Januari 24 mwaka huu katika eneo la Namba mmoja lilipo katika pori hilo kinyume na kifungu namba 15 (1)(2) sura ya 5 ya sheria ya wanayamapori ya mwaka 2009.
Shitaka la pili la kuchimba mchanga unaodhaniwa kuwa na dhahabu Emmanuel amekiuka kifungu namba 1,2,4 sura ya 5 ya sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009.
Emmanuel tayari ameanza kutumikia adhabu yake baada ya kushindwa kulipa gharama zilizotolewa katika Hukumu yake.