Mhasibu wa Wizara ya Afya, Luis Lyimo (54) na Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Christian Social Services Commission, Peter Maduki (61) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka 280 yakiwemo 150 ya kughushi na moja la kutakatisha fedha.
Mawakili wa Serikali , Zakaria Ndaskoi na Genes Tesha wamewasomea mashtaka washtakiwa hao jana Jumatatu Januari 6, 2020 huku wakipokezana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando.
Wakili Ndaskoi amedai washtakiwa hao walitenda makosa hayo kati ya mwaka 2017 na mwaka 2019 ndani ya Jiji la Dar es Salaam
Alidai washtakiwa hao kwa nafasi zao wakiwa na nia ovu walighushi hundi mbalimbali zenye thamani ya mamilioni ya fedha na kusaini kwa jina la Upendo Mwingira bila ridhaa yake huku wakijaribu kuonyesha mshtakiwa, Luis Lymo alikuwa akilipwa na taasisi ya Christian Social Services Commission Fedha hizo kama kamisheni wakati si kweli.
Katika mashtaka ya kuwasilisha nyaraka za uongo washtakiwa hao wanadaiwa kuwasilisha nyaraka mbalimbali walizozighushi katika benki ya Standard Chartered.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa hao hawakuruhusiwa kuongeza chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikilizwa kesi ya uhujumu uchumi.
Upande wa mashtaka ulidai upelelezi bado haujakamilika, washtakiwa walipelekwa rumande na kesi imeahirishwa mpaka Januari 20 2020
Social Plugin