MKURUGENZI MKAZI WA BENKI YA DUNIA ANAYEMALIZA MUDA WAKE BI.BELLA BIRD APONGEZA TASAF KWA MAFANIKIO YA KUPUNGUZA UMASKINI NCHINI

 Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Bw. Ladislaus Mwamanga  (picha ya juu na chini ) akimkabidhi zawadi Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia anayemaliza muda wake nchini Bi. Bella Bird katika hafla ya kuagana naye .
 
 Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga (aliyesimama) akizungumza wakati wa hafla fupi ya kuagana na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia aliyemaliza muda wake, Bi. Bella Bird alipofika kwenye ofisi ndogo za Mfuko huo jijini Dar es Salaam kuagana na wafanyakazi wa taasisi hiyo.
 Baadhi ya wafanyakazi wa TASAF wakimsikiliza Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird (hayupo pichani ) wakati alipofika katika taasisi hiyo kuagana nao baada ya kumaliza muda wake nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF bw.Ladislaus Mwamanga (aliyevaa tai) akimwongoza Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia anayemaliza muda wake bi. Bella Bird kuingia katika ukumbi wa mikutano wa TASAF katika ofisi ndogo jijini Dar es Salaam.


Na Estom Sanga- TASAF- DAR ES SALAAM

Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia anayemaliza muda wake Bi.Bella Bird amepongeza jitihada za serikali ya Tanzania kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii- TASAF- kwa hatua inazoendelea kuchukua katika kukabiliana na umaskini nchini.

Bi.Bella Bird amesema Tanzania imepata mafanikio makubwa katika azma ya kuwaondolea wananchi wake kero ya umaskini jambo ambalo amesema limeijengea heshima kubwa serikali na hivyo kufanya mataifa mengine hususani ya bara la Afrika kuwavutiwa nayo.

Mkurugenzi Mkazi huyo wa Benki ya Dunia anayemaliza muda wake ameyasema hayo alipokutana na Wafanyakazi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF- katika Ofisi ndogo ya Mfuko huo jijini Dar es salaam ambako alikwenda kuagana nao baada ya kumaliza kipindi chake cha takribani CHA utumishi wa miaka minne hapa nchini.

‘’ mataifa mengine ya Afrika yamekuwa yakija Tanzania kujifunza namna TASAF ilivyofanikiwa kuwafikia watu maskini kabisa kupitia Mpango wake wa Kunusuru Kaya Maskini’’ amesisitiza Bi. Bella Bird.

Amesema tafiti huru za ndani na nje ya nchini zilizofanywa zinaonyesha kuwa umaskini nchini Tanzania umepungua katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na kuwa kinachotakiwa sasa ni kuhakikisha kuwa mafanikio hayo yanalindwa, kuboreshwa na kuendelezwa.

Bi.Bella Bird amesisitiza kuwa Benki ya Dunia itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa miradi inayolenga kuboresha maisha ya wananchi na kuongeza kuwa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Serikali kupitia TASAF ni miongoni mwa miradi hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo fupi Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuweka mazingira yaliyosaidia Benki ya Dunia kukubali kufadhili shughuli za Mpango was Kunusuru Kaya Maskini.

Bwana Mwamanga amesema mafanikio makubwa yaliyopatikana katika utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ya sehemu ya kwanza yamewezesha Serikali kukubali kutekeleza sehemu ya pili ambayo inatarajiwa kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli baadaye mwezi ujao.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF ameahidi kuwa taasisi hiyo imejipanga vizuri kuhakikisha kuwa sehemu ya pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini inatekelezwa kwa ufanisi mkubwa kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali huku Mkazo ukiwekwa katika kuwashirikisha Walengwa katika kutekeleza miradi ya Maendeleo kwenye maeneo yao na kisha kulipwa ujira kama sehemu ya kuwaongezea kipato .

Utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF ulianzishwa na Serikali kwa lengo la kusaidia wananchi kupitia utaratibu wa Kaya Maskini sana ili ziweze kujikimu kwa kupata mahitaji muhimu yakiwemo lishe, elimu na afya huku mkazo ukiwekwa katika kuziwezesha kaya za Walengwa kutumia sehemu ya ruzuku kuanzisha miradi midogo midogo ya uzalishaji mali ili kuinua kipato chao na kuboresha maisha yao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post