Moja ya mashine za Radiolojia za vipimo vya MRI zilizopo Hospitali za Serikali hapa Nchini.
Na Andrew Chale, Arusha
HOSPITALI ya Rufaa ya Mount Meru, mkoani hapa ina mpango wa kuanzisha huduma za vipimo vya MRI na CT-Scan ili kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.
Akizungumza Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dkt. Shafii Msechu, wakati akizungumza na waandishi wa habari na maofisa mawasiliano wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, katika kampeni yake ya 'Tumeboresha Sekta ya Afya'.
Lengo la ziara hiyo ni kuangazia mafanikio ya Serikali yaliyopatikana katika sekta ya afya kwa kipindi cha miaka minne.
Alisema miongoni mwa mipango ya Hospitali ni kuona huduma za kibingwa ikiwemo vipimo hivyo vya MRI na TC- scan vinasogezwa karibu.
"MRI na TC-Scan ni vipimo vya gharama. Huduma hizi kwa sasa hakuna na zinatolewa nje ya hapa. Mpango ni kuwa na mashine hizi na kutoa huduma karibu na wananchi ilikuwapunguzia gharama za kufuata mbali" alisema Dkt. Msechu.
Huduma hiyo kwa sasa inatolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC.
Dkt. Msechu aliongeza kuwa wapo mbioni kuanzisha huduma za usafishaji wa figo.
Huduma hiyo inatarajiwa kuanza mra baada ya kukamilika kwa ujenzi wa jengo litakalogharimu Sh. millioni 600.
Kwa sasa upimaji wa eneo la ujenzi wa jengo la kutolea huduma hiyo, umekamilika na wanasubiri fedha kutoka Serikali ili kuanza ujenzi huo.
"Hospitali ya Mount Meru inatarajia kuanza kutoa huduma za usafishaji wa figo na tayari tuna mashine tano za kuanza kutoa huduma hii tulizopewa na Wizara na wadau wa afya na tunachosubiri ni fedha za kuanza ujenzi," alisema Dkt. Msechu.
Alibainisha kuwa, kuanzisha huduma hiyo ni kutokana na kuwapo kwa wagonjwa wenye matatizo hayo lakini kutokana na kutokuwa na huduma hiyo wamekuwa wakiwapeleka hospitali nyingine.
Dk. Msechu alisema kwa mwezi wanapokea wagonjwa watatu wa Figo wanawahamishia katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC.
Hospitali hiyo imekuwa ikitoa huduma mbalimbali za matibabu huku kwa siku wanapokea wagonjwa wapya 320 hadi 500, wa marudio 250 hadi 350 na watoto 30 hadi 50.
Pia wana Madaktari bingwa wa kufanya upasuaji na asilimia 34 wanawafanyiwa wajawazito ambao idadi yao ni 200 kila mwezi.
Kadhalika alisema wanatoa msamaha wa matibabu ya wagonjwa 3,224 kwa mwezi na wanagharamia Sh. milioni 41.8.