Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Picha :MZEE ALMASI "MWENZANGU " AFARIKI DUNIA...MSIBA WAKE UTATA MTUPU, SERIKALI YATOA MSIMAMO

Mzee John Shija Tuju (72) maarufu Mzee Almasi ama ‘MWENZANGU / Iduguye’ enzi za uhai wake.
Mzee John Shija Tuju (72) maarufu Mzee Almasi ama ‘MWENZANGU’ enzi za uhai wake.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog 

Kumetokea sintofahamu ya mazishi ya Mzee John Shija Tuju (72) maarufu Mzee Almasi ama ‘MWENZANGU / IDUGUYE’ kutokana na mtindo wa uombaji pesa aliokuwa anautumia Mjini Shinyanga baada ya serikali ya sasa ya mtaa wa Ngokolo kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga kudai haitambui mzee huyo kama mkazi wa eneo hilo hivyo kukwamisha shughuli za mazishi.



Wakati serikali ya mtaa iliyopo ikisema haimtambui mzee huyo aliyefariki dunia Januari 8,2020 majira ya saa 11 jioni baada ya kuanguka ,mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo aliyepita John Nangi amesema mzee huyo ni mkazi wa eneo hilo na amekuwa akihudhuria misiba japokuwa huwa hachangii pesa.



Taarifa kutoka mtaa wa Ngokolo zinasema Mzee huyo ambaye alikuwa mlemavu wa viungo ‘mguu mmoja’ aliyekuwa anaishi kwa Kuomba Omba Mjini Shinyanga alikuwa anadaiwa Shilingi 18,000/= na mtaa wake kwa ajili ya kununua vifaa mbalimbali vinavyotumiwa wakati wa misiba.

Inaelezwa kuwa kutokana na deni hilo viongozi wa mtaa huo waliamua kujitenga naye kutokana na kukiuka taratibu za mtaa huku wakidai kuwa Mzee huyo hakuwa amejiorodhesha kwenye daftari la mtaa.

Kwa Mujibu wa mpangaji mwenzake na marehemu, James Lumanyika amesema tangu utokee msiba wa Mzee Almasi Januari 8,2020 hakuna mwananzengo yeyote aliyefika msibani na kila wanapofuatilia kwa viongozi wa mtaa hakuna anayetoa sababu zinazoeleweka zaidi ya kuambiwa marehemu hakuwa mwana mtaa na alikuwa anadaiwa shilingi 18,000/=.

Kwa upande wake mtoto wa marehemu Emmanuel Charles licha ya serikali ya mtaa kusema haimtambui marehemu aliomba asaidiwe kufanikisha mazishi ya baba yake na kuelezwa kuwa familia imekubaliana marehemu akazikwe katika kijiji cha Mwalugoye katika kata ya Chibe.

Akizungumza na Malunde1 blog Mwenyekiti wa Mtaa wa Ngokolo Thomas Joseph Ng’ombe amesema hamtambui Mzee huyo kama mkazi wa Ngokolo kwani alikuwa hajajiorodhesha kwenye daftari la mtaa na alikuwa hahudhurii kwenye misiba.

"Tulipata taarifa za msiba wa Mzee huyu jana Januari 9,2020 na tulikuwa tunaendelea kufuatilia ili kuangalia namna ya kusaidia mazishi yake",alisema Ng'ombe.

Naye Mwenyekiti wa Nzengo ya Ngokolo,Silvester Senga amesisitiza kuwa Mzee Almasi/Charles hakuwa kwenye kitabu cha mtaa na kwamba hakuwahi kumuona kwenye mtaa huo na hajawawahi kujitambulisha kwenye nzengo hivyo anachofanya yeye ni kutekeleza utaratibu uliowekwa na mtaa.

Hata hivyo taarifa za serikali ya mtaa kutomtambua mzee huyo zimepingwa vikali na Aliyekuwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Ngokolo John Nangi Masoud ambaye amesema anamtambua mzee huyo kwani amekuwa akiishi na familia yake kwenye mtaa huo kwa kipindi kirefu.

“Mzee Almasi ni mkazi wa mtaa huu.Viongozi wa mtaa wanasema kwamba wananchi wamegomea msiba,hii siyo kweli. Mimi nasema Viongozi wa serikali ya mtaa ndiyo wamegomesha msiba huu. Wanajaribu kukwepa tu. Mzee wetu alikuwa mhudhuriaji mzuri wa misiba tatizo lake ni kwamba yeye huwa hana pesa kwa sababu alikuwa anaishi kwa kuomba omba”,alieleza Nangi.

Kutokana na mkanganyiko huo, Afisa Mtendaji wa Kata ya Ngokolo,Felister Msemelwa ameagiza serikali ya mtaa kumpatia stahiki zote za mazishi marehemu.

“Natoa tamko sasa ni kwamba ndugu yetu apatiwe stahiki za mtaa,ahudumiwe kama vile mmekuwa mkiwahudumia wengine katika mtaa huu. Mtendeeni yale yote anayopaswa kutendewa. Marehemu alikuwa mlemavu na taarifa za makazi ya ndugu yetu zimepishana kati ya serikali iliyopo na iliyopita”,alisema Msemelwa.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ngokolo Mhe. Emmanuel Ntobi alisema kitendo cha kugomea mazishi ya Mzee Almasi ni kukiuka katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuiomba wananzengo wamsiri mzee huyo.

“Naomba Nzengo izingatie utu tumsitiri kwanza Mzee wetu ndiyo tujadili mengine. Mzee huyu alikuwa Omba omba huyu anaingia kwenye kundi maalumu badala ya kumuingiza kwenye kundi la watu wa kawaida. Mwili utaagwa hapa Ngokolo na utazikwa Chibe baada ya kukosa ushirikiano hapa Ngokolo”,alisema Ntobi.

Nao wakazi wa mtaa wa Ngokolo wameeleza kusikitishwa na kitendo cha viongozi wa serikali ya mtaa kugomea msiba huo wakisema kitendo hicho kinakiuka haki za binadamu huku wengine wakiwataka viongozi kuacha kubagua wananchi wasio na uwezo.

"Viongozi mnafanya hivi kwa sababu Mzee Almasi alikuwa maskini,ombaomba?,angekuwa amefariki dunia tajiri hapa mngekuwa tayari mmeshachukua hatua",alisema Chacha.

Mzee Almasi ambaye ni Omba omba maarufu Mjini Shinyanga atakumbukwa kwa mtindo wa uombaji pesa aliokuwa anautumia ikiwemo "Samahani Mwenzangu nisaidie Ka hela",  "Kijana wangu Hujambo! nisaidie Ka hela", "Kijana wangu naomba hata ka mia tano", "Chenji ninayo"

ANGALIA PICHA HAPA
 Afisa Mtendaji wa Kata ya Ngokolo,Felister Msemelwa akiagiza serikali ya mtaa wa Ngokolo kumpatia stahiki zote za mazishi marehemu John Shija Tuju (72) maarufu Mzee Almasi ama ‘MWENZANGU’ leo Januari 10,2020 . Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mwenyekiti wa Mtaa wa Ngokolo Thomas Joseph Ng’ombe akiwaeleza waandishi wa habari kuwa hamtambui marehemu John Shija Tuju (72) maarufu Mzee Almasi ama ‘MWENZANGU’ kama mkazi wa Ngokolo kwani alikuwa hajajiorodhesha kwenye daftari la mtaa na alikuwa hahudhurii kwenye misiba.
Mwenyekiti wa Nzengo ya Ngokolo,Silvester Senga akisisitiza kuwa John Shija Tuju (72) maarufu Mzee Almasi ama ‘MWENZANGU’ hakuwa kwenye kitabu cha mtaa na kwamba hakuwahi kumuona kwenye mtaa huo na hajawawahi kujitambulisha kwenye nzengo.
Mtoto wa marehemu Emmanuel Charles akielezea kuhusu msiba wa baba yake John Shija Tuju (72) maarufu Mzee Almasi ama ‘MWENZANGU’
 Mpangaji mwenzake na marehemu, James Lumanyika akielezea kuhusu msiba wa John Shija Tuju (72) maarufu Mzee Almasi ama ‘MWENZANGU’
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Ngokolo John Nangi Masoud alielezea kuhusu msiba wa Mzee Almasi. Alisema anamtambua mzee huyo kwani amekuwa akiishi na familia yake kwenye mtaa huo kwa kipindi kirefu.
Diwani wa Kata ya Ngokolo Mhe. Emmanuel Ntobi akielezea kuhusu msiba wa Mzee Almasi ' Mwenzangu' ambapo alisema kitendo cha kugomea mazishi ya Mzee Almasi ni kukiuka katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuiomba wananzengo wamsiri mzee huyo.
Mkazi wa Mtaa wa Ngokolo Chacha akiwataka viongozi wa serikali ya mtaa kuacha kubagua wananchi maskini na tajiri.
Sehemu ya wakazi wa Mtaa wa Ngokolo waliofika nyumbani kwa mzee Almasi ' Mwenzangu' leo asubuhi.
Sehemu ya wakazi wa Mtaa wa Ngokolo waliofika nyumbani kwa mzee Almasi ' Mwenzangu' leo asubuhi.
Picha na Kadama Malunde - Malunde - Blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com