WANANZENGO WAGOMBANIA KITI KIMOJA MSIBANI MAJENGO KAHAMA MJINI



Kiti pekee kinachotumiwa na wakazi wa mtaa wa Majengo Kahama Mjini kwenye matukio ya misiba



Na Adela Madyane-Malunde 1 blog Kahama

Mgogoro baina ya Wananchi wa Mtaa wa Majengo na viongozi wa mtaa huo umeibuka baada ya Nzengo hiyo kupatwa na msiba hapo jana na kukosa viti vya kukalia, huku nzengo nzima ikimiliki kiti kimoja pekee.

Mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu sasa, umekuwa ukitokea mara tu panapokuwa na msiba katika nzengo hiyo kutokana na uwepo wa kiti kimoja ambacho hakikidhi mahitaji ya umati unaokuwa umehudhuria msibani.

Wananchi waliohudhuria msiba huo walisema mgogoro huo umesababishwa na viongozi wa mtaa kushindwa kuhamasisha wananchi kuchangia ununuzi wa viti jambo ambalo linapelekea kila unapotokea msiba katika eneo lao mgogoro kuibuka juu la suala la kukosekana kwa viti kwa nzengo hiyo. 

“Hili tatizo la ukosefu wa viti ni la muda mrefu sasa na linakera. Tumemhoji mwenyekiti wa mtaa mara kadhaa na binafsi nimeona tatizo lipo kwa viongozi wetu wa mtaa kwani wananzengo hawawezi kushindwa kuchangia ununuzi wa viti,” alisema James Magini mkazi wa mtaa wa Majengo kati.

Naye Joramu Jumanne alisema ili kumaliza mgogoro huo viongozi wa Mtaa kwa kushirikiana na viongozi wa Nzengo wanapaswa kutoa elimu kwa wananchi juu ya ununuzi wa viti pamoja na vitu vingine kama maturubai, na sio kuwalazimisha kutoa michango ya kununua viti pindi msiba unapotokea kwani kwa kufanya hivyo shida inaweza kutokea.

“Changamoto zipo nyingi katika mtaa wa Majengo Kati zinazohitaji vikao vya dharula ili viongozi na wananchi wakae meza moja kulipatia ufumbuzi kwani ni muda mrefu Nzengo ina kiti kimoja atakayekiwahi ndiyo huyo na hapa tuna watu wa kada mbalimbali katika nyadhifa mfano akija mkuu wa Wilaya msibani mwananchi aliyekalia hicho kiti atalazimika kukiachia bila kujali umri,” alisema Joramu.

Naye Balozi wa Nzengo ya Majengo Kati Donald Masele akizungumza na waandishi wa Habari waliofika katika tukio hilo alikiri na kusema kuwa uzembe unasababishwa na wao viongozi kushindwa kuweka mkazo kwa wananchi juu ya uchangiaji wa viti jambo ambalo linazusha mgogoro.

“Viongozi tukiwa na mkazo viti vitapatikana kwenye nzengo yetu kwani wananchi wapo tayari kuchangia lakini kumekuwa na uzembe katika kufanya ufuatiliaji, na uzembe huu umesababishwa na wanakamati waliokabidhiwa kusimamia jukumu hilo", alisema Masele Balozi wa Majengo Kati.

Masele aliongeza  kuwa wakazi wa Majengo Kati wana pesa na wanamiliki miradi mikubwa ya maendeleo hivyo hawawezi kushindwa kuchangia kiti kimoja kwa kaya moja kwa thamani ya elfu 15,000/=.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo John Lwaga Kitambi alisema Mtaa wake una nzengo zaidi ya tano alianza kuhamasisha uchangiaji wa viti Majengo Kati na Majengo Mashariki na kubainisha kuwa Nzengo hizo mbili mwitikio ni mbovu.

Alisema kuwa hatua itakayochuliwa kwa wananchi watakaokaidi kuanzia sasa juu ya michango itokanayo na misiba ni kutunga sheria ndogo ndogo itakayodhibiti hali hiyo ili wakienda tofauti hatua kali itachukuliwa dhidi yake.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post