Na Saada Akida, ZANZIBAR
MTIBWA Sugar ndio mabingwa wa Kombe la Mapinduzi mwaka 2020, baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya mabingwa wa Tanzania, Simba SC usiku huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, kiungo Awadh Salum Juma, mchezaji wa zamani wa timu ya vijana ya Yanga na African Lyon kipindi cha kwanza.
Na hilo linakuwa taji la pili la Kombe la Mapinduzi kwa Mtibwa Sugar baada ya awali kulibeba mwaka 2010 wakiifunga Ocean View katika fainali, lakini pia Wakata Miwa hao wa Manungu wamelipa kisasi cha kufungwa na Simba kwenye fainali mwaka 2015.
Awadh, kijana mwenye nguvu na kasi, alifunga bao hilo dakika ya 38 akimalizia pasi ya kurudishiwa na Jaffar Kibaya baada ya yeye mwenyewe kutoka na mpira nyuma pembeni kushoto akiwapita wachezaji wa Simba.
Bao hilo halikuonekana kuwavuruga kabisa Simba SC walio chini ya kocha Mbelgiji, Sven Ludwig Vandenbroeck na wakaendelea kucheza kwa kushambulia na kwa kujiamini.
Lakini kipindi cha pili Vandenbroeck aliyejiunga na Simba Desemba tu baada ya kufukuzwa kwa Mbelgiji mwenzake, Patrick Aussems alikianza na mabadiliko ya wachezaji wanne, akiwatoa mabeki Haruna Shamte, Mbrazil Toirone Santos na viungo Said Ndemla na Rashid Juma na kuwaigingiza Nahodha na mshambuliaji John Bocco, beki Muivory Coast Pascal Wawa na viungo Ibrahim Ajibu na Mkenya Francis Kahata.
Hata hivyo, mabadliko hayo hayakuweza kupindua matokeo na zaidi mlinda mlango Beno Kakolanya aliendelea kuwa mtu muhimu kwa kuokoa hatari kadhaa langoni mwake.
Hii ni mara ya tatu ndani ya miaka minne, Simba SC wanangia fainali ya Kombe la Mapinduzi lakini wanafungwa baada ya 2017 na 2019 kuchapwa na Azam FC mar azote mbili.
Kikosi cha Mtibwa Sugar kilikuwa: Shaaban Kado, Dickson Job, Jaffary Kibaya, Cassian Ponera, Salum Kihimbwa/Omary Sultan dk68, Ally Makarani, Awadhi Juma, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Abdulhalim Humud, Onesmo Mayaya/Haroun Chanongo dk61 na Kibwana Shomari.
Simba SC: Benno Kakolanya, Haruna Shamte/John Bocco dk75, Gardiel Michael, Toirone Santos/Pascal Wawa dk46, Said Ndemla/Ibrahim Ajibu dk59, Rashid Juma/Francis Kahata dk46, Clatous Chama, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Miraji Athuman/Hassan Dilunga dk37 na Meddie Kagere.
Chanzo- Binzubeiry blog
Social Plugin