Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack (kushoto) na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Jasinta Mboneko wakimhoji mtoto Majebele Masanja baada ya kumkuta akichunga ng'ombe muda wa masomo hapo jana tarehe 07/01/2020 eneo la shule ya Sekondari Ilindi, kata ya Zongomela Wilaya ya Kahama.

***
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amemtaka Mwenyekiti wa kijiji cha Ilindi, kata ya Zongomela kuhakikisha mtoto Majebele Masanja anaacha mara moja kazi ya kuchunga ng’ombe na anapelekwa shule.
Mhe. Telack ametoa agizo hilo jana tarehe 07/01/2020 baada ya kumkuta mtoto huyo maeneo ya shule ya Sekondari Ilindi akiwa anachunga ng’ombe badala ya kuwa shuleni ambapo alihojiwa na kusema kuwa anafanya kazi kwa ujira wa sh. 20,000 kwa mwezi na kuwa hasomi kwa sababu mzazi wake hana uwezo.
Akizungumza na Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji wa Halmashauri ya Mji Kahama katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo ambapo ametoa agizo hilo kwa Mwenyekiti huyo, Telack amesema wenyeviti wote wakahakikishe wazazi wanaelekezwa kusimamia mahudhurio ya wanafunzi shuleni.
“Mkazungumze na wananchi, wazazi na walezi kuhusu wanafunzi wasiofika shuleni, mkafanye mikutano ya hadhara na muazimie kusimamia mahudhurio shuleni” amewaambia.
“Haiwezekani wazazi kuacha watoto wanachunga badala ya kusoma, mtoto yule apelekwe shuleni na nitafuatilia” amesema Mhe. Telack.
Aidha, Telack amewasisitiza Wenyeviti wote wa Mitaa na Vijiji kushirikisha wananchi katika shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na kujenga maboma ya madarasa, kusaidia kukomesha matumizi ya madawa ya kulevya na kuwaongoza wananchi bila kuendekeza migogoro isiyokuwa na sababu.
Social Plugin