Amina Ayoub (7) aliyepotea siku mbili zilizopita amekutwa amekufa leo Jumatatu Januari 27, 2020 katika eneo la Pugu Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam huku mwili wake ukinyofolewa sehemu za siri na macho.
Ndugu wa mtoto huyo waliwasiliana na gazeti la Mwananchi ili kutoa tangazo la kupotea kwake lakini kabla ya tangazo hilo kutoka, wakapata taarifa za kifo hicho.
Akizungumza na Mwananchi leo, Mwita John anayeishi jirani na alipokuwa akiishi mtoto huyo amesema Amina alitoweka Ijumaa iliyopita Januari 24, 2020.
“Tukishirikiana na familia yake tulimtafuta Amina bila mafanikio. Lakini (jana) tulipiga simu ofisi za Mwananchi kwa ajili ya kupata utaratibu wa kutoa tangazo kuhusu kupotea kwake ambalo lilitakiwa litoke leo.”
“Tukiwa katika jitihada hizo za kutaka kutoa tangazo jirani yetu akatueleza kuwa siku ya Ijumaa alisikia sauti zikitokea katika pori, akatushauri tuingie tukamsake huenda akawa Amina tunayemtafuta,” amesema John.
John amesema jirani yao anayeishi karibu na pori hilo aliwaeleza hayo baada ya kusikia taarifa za familia hiyo kumtafuta Amina, walipokwenda ofisi za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupata kibali cha kuingia katika pori hilo, walitakiwa kutoa taarifa polisi.
Amebainisha kuwa baada ya kufuata taratibu zote leo saa 5 asubuhi waliingia katika pori hilo na kuukuta mwili wa Amina ukiwa umenyofolewa sehemu za siri na kutobolewa macho.
“Hivi ni baadhi ya vitu tulivyoviona, kifo chake kinasikitisha sana. Tuna wasiwasi baba yake wa kufikia anahusika na suala hili, hata hivyo tayari polisi wameshamkamata kwa ajili ya mahojiano,” amesema John.
Via Mwananchi