Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MV- MWANZA KUSTAWISHA BIASHARA KANDA YA ZIWA, NA NCHI JIRANI ZA KENYA NA UGANDA

Na.Paschal Dotto-MAELEZO.

Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mingi ya kuimarisha miundombinu katika sekta mbalimbali ikiwemo mradi ya umeme (JN HPP-Julius Nyerere Hydropower project) kwa gharama ya shilingi trilioni 6.5, Ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR kwa gharama ya shilingi trilioni 7 na miradi mingine ambayo itaweka mazingira wezeshi kwa wananchi kufanya biashara na uwekezaji.

Mnamo Desemba 8, 2019, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli alizindua ujenzi wa mradi mwingine mkubwa wa ujenzi wa meli kubwa ya abiria na mizigo ya MV. Mwanza, ukarabati wa meli za MV. Victoria na MV. Butiama pamoja na ujenzi wa chelezo katika lango la biashara na uchumi kanda za ziwa ambao utekelezaji wake unaendelea vizuri na utakapokamilika utakuwa umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 153.7.

Meneja wa mradi huo, Mhandisi Abel Gwanafyo ameeleza kuwa, meli kubwa ya “MV Mwanza, Hapa Kazi Tu” itakayogharimu shilingi bilioni 89.76 ambayo ujenzi wake unatekelezwa na kampuni ya ujenzi ya GAS ENTEC wakishirikiana na KANG NAM kutoka Korea Kusini pamoja na SUMA JKT kutoka Tanzania, itakuja kuwa mbadala ya Meli ya MV Bukoba ambayo ilizama miaka 23 ilipita.

 Katika kampeni za uchaguzi mkuu wa 2015, Rais wa Awamu ya Tano, Dkt John Pombe Magufuli aliwaahidi wananchi wa kanda ya ziwa kuwa atajenga meli kubwa kuwaenzi waliokufa kwenye ajali hiyo lakini pia kuimarisha usafirishaji katika ukanda huo wa Tanzania kwani kuna fursa nyingi za biashara.

“Ni miaka 23, tangu kuzama meli ya MV. Bukoba mwaka 1996, miaka mingi imepita, lakini pia kuharibika kwa meli ya mizigo kumekuwa na tatizo kubwa kwa sekta ya usafarishaji kwa wananchi wanaioshi kuzunguka ziwa Victoria na hivyo kuathiri shughuli za uchumi na uzalishaji Kanda ya Ziwa”, Rais Dkt. John Magufuli.

Mradi huo mkubwa utakwenda sambamba na miradi mingine ya ukarabati wa meli ya Mv Victoria utaogharimu shilingi bilioni 22.71, Mv Butiama bilioni 4.9, ambazo ujenzi wake unatekelezwa na kampuni ya ujenzi ya KTMI kutoka Korea Kusini huku ujenzi wa chelezo utakaogharimu shilingi bilioni 36.4, unatekelezwa na kampuni ya Stx Engine ikishirikiana na SAE Kyong kutoka Korea Kusini.

MV Mwanza Hapa Kazi Tu, itakuwa na urefu wa mita 92, na uwezo wa kubeba abiria 1,200, mizigo tani 400, magari makubwa 3 na magari madogo 20, huku Mv Victoria ikibeba abiria 1,200, mizigo tani 200 na Mv Butiama abiria 200, tani 100, na kuwezesha zaidi ya abiria 2,600 na tani 700 za mizigo kwa wakati mmoja hivyo kusadia kupunguza adha ya usafiri na usafirishaji kwa abiria na mizigo katika ukanda huo wa ziwa.

“Ni wazi kuwa utekelezaji wa miradi hii utakaogharimu shilingi bilioni 153.7 utasaidia sana kutatua tatizo la usafiri na usafirishaji kwa wananchi wanaoishi kando ya ziwa Victoria, siyo tu hapa nchini bali hata kwa jirani zetu Kenya na Uganda kwa hiyo ni miradi ambayo ina manufaa kwa uchumi wetu”, amesema Rais Magufuli.

Aidha kukamilika kwa mradi huu kutaondoa kwa kiasi kikubwa tatizo la usafiri kwa abiria katika ukanda huo wa ziwa ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa mizigo na mazao mbalimbali ya biashara na kuzalisha ajira kwani meli hii itahitaji wafanyakazi wa aina mbalimbali. Kwa upande wa nchi jirani za Kenya na Uganda , hii pia itakuwa fursa kwao kusafirisha mazao ya biashara na chakula kupitia ziwa Victoria badala ya kutegemea usafiri wa aina moja wa barabara au wa anga.

 Katika uzinduzi wa ujenzi wa mradi huo ambao utafungua ukanda wa kibiashara na kusaidia kukuza pato la taifa, Rais Magufuli alieleza dhamira kubwa ya Serikali ya Awamu ya Tano kuwa ni kufanya mabadiliko makubwa kwa kuleta miradi wezeshi kwa wananchi bila kutegemea misaada yenye masharti lukuki na ufadhili.

Sekta hii ya usafirishaji kwa njia ya maji ni muhimu sana na Serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzani (TPA), pamoja na Shirika la Huduma za Meli imekuwa na usimamizi madhubuti ili kukuza  na kuimarisha sekta hiyo ambayo ni nyenzo kubwa katika uchumi.

Kampuni ya Huduma za meli iliyoanzishwa na Baba wa Taifa, Mwl. Julius Nyerere kwa sasa inafanya kazi kubwa baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani na kuelekeza nguvu katika kuimarisha bandari nchini. Hapo awali ziwa Victoria lilikuwa meli 14 ikiwemo meli ya utalii, lakini meli hiyo iliacha kufanya kazi kutokana na uongozi mbovu, ikiwa ni pamoja na vitendo vya wizi na ubadhilifu wa mali za umma  na hatimaye meli zote 14 ziliisha na kubaki moja tu.

“Nawapongeza Kampuni ya Huduma za Meli kwa kuboresha utendaji kazi katika kampuni hii, kwani miaka ya nyuma hata mishahara mlikuwa hamuwezi kulipa wafanyakazi wenu, lakini kwa sasa utendaji kazi uko vizuri na umeimarika ambapo mpaka sasa meli nne zipo na zinafanya kazi. Meli hizo ni Mv Clarius, Mv Umoja, Mv Sangara na Mv Wimbi, kwa hiyo ujenzi wa meli mpya na ukarabati wa meli hizi mbili utasaidia kukuza huduma zenu”, alisema,Rais Magufuli.

Mamlaka ya Bandari imekuwa ikiendelea na upanuzi na ujenzi wa bandari mbalimbali nchini zikiwemo bandari ya Dar es Salaam, Mtwara, Tanga, Mwanza na bandari zake ndogondogo za Kemendo, Bukoba, Kwemukwikwi na Nyamirembe kwa upande wa kanda ya ziwa.

 Mhandisi,Gwanafyo ameeleza kuwa ujenzi wa meli mpya “Mv Mwanza Hapa Kazi Tu” umefikia asilimia 52 tofauti na mwezi Desemba 2019 ambapo ulikuwa asilimi 50, huku ukarabati wa Mv Victoria ukiwa asilimia 75 badala ya 65, Mv Butiama asilimi 70 badala ya 60 huku ujenzi wa chelezo ukiwa ni asilimia 80 badala 68 za mwezi Desemba 2019.

Miradi hiyo imeweza kutoa fursa nyingi kwa wananchi wa mkoa wa Mwanza ikiwemo fursa za biashara na ajira kwani mpaka sasa kuna ajira zaidi ya 1,000 na bado zinaongezeka kwa kadri siku zinavyoongezeka.

Ujenzi wa meli hii kubwa ni utekelezaji wa ahadi na kutimiza maono ya Baba wa Taifa Mwl.Julius Nyerere aliyetaka kuwepo na meli kubwa katika ukanda huo wa kiuchumi wa Tanzania, ambapo mwaka 1979, alisimamia kuundwa kwa  meli ya MV Bukoba ambayo  ilizama mwaka 1996 na kuleta ugumu wa usafiri na usafirishaji katika ziwa Victoria ambalo ni tegemeo kwa wananchi wa kanda hiyo pamoja na nchi jirani. Uamuzi wa  Rais Magufuli wa kujenga meli hiyo kubwa ‘Mv Mwanza, Hapa Kazi Tu’ na kukarabati meli nyingine unaonyesha jinsi alivyodhamiria kuyaishi na kuyatekeleza maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwa vitendo.

Mwisho



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com