Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Mwekezaji kutoka nchini India, Bw.Vivek Agarwala ameonesha nia ya kuwekeza kwenye kilimo cha mpunga kupitia umwagiliaji na kujenga kiwanda cha kuchakata mpunga wilayani Busega mkoani Simiyu, ambapo anatarajia kuwekeza katika eneo lenye ukubwa wa ekari zipatazo 2000.
Akizungumza na viongozi na watendaji wa Mkoa wa Simiyu baada ya kutembelea maeneo mbalimbali yenye fursa ya uwekezaji katika kilimo cha mpunga wilayani Busega, Bw. Agarwala amesema mkoa wa Simiyu na Tanzania kwa ujumla ina rasilimali nyingi hivyo ikiwa Makampuni kutoka India yatafanya kazi kwa kushirikiana na Watanzania rasilimali hizo ziatakuwa na manufaa kwa Watanzania.
“Mkoa wa Simiyu na Tanzania kwa ujumla ina rasilimali za kutosha ambazo zipo kwa ajili ya kuwanufaisha Watanzania wenyewe hivyo kinachohitajika ni teknolojia, uwekezaji, ushirikiano kutoka Serikalini kufanya haya yote yatokee; baada ya ziara hii ninaamini tukiyatekeleza kwa juhudi yale tuliyokubaliana mkoa huu utaendelea kwa kasi,” alisema Agarwala.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amemhakikishia mwekezaji huyo upatikanaji wa eneo la ekari 2000 kwa ajili ya uwekezaji na kubainisha kuwa malengo ya mkoa ni kuhakikisha wilaya ya Busega inakuwa mzalishaji mkuu wa chakula katika mkoa kwa kuwa ndiyo wilaya yenye ziwa Victoria ndani ya Mkoa.
Aidha, pamoja na kutoa ushirikiano kwa mwekezaji kutimiza azma yake Mtaka amesema Serikali ya Mkoa imezungumza na Benki ya CRDB kuona uwezekano wa kuwawezesha wakulima wa mpunga wilayani Busega hususani walio kando ya ziwa Victoria kupitia dirisha la kilimo ili waweze kulima kisasa kupitia umwagiliaji.
Naye Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Ziwa, Bw. Lusingi Sitta amesema Benki iko tayari kumuunga mkono mwekezaji na wakulima wa wilaya ya Busega kupitia dirisha la kilimo kutokana na wilaya hiyo kuwa na maeneo mazuri na chanzo cha uhakika cha maji (Ziwa Victoria), ambapo alibainisha kuwa tayari benki hiyo ina uzoefu wa kuwezesha miradi mbalimbali ya kilimo cha umwagiliaji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu, Mhe. Enock Yakobo amesema wao kama chama wanaunga mkono juhudi za watu wanaoitika huku akiongeza kuwa mkoa huo ni miongoni mwa mikoa inayofanya vizuri kwenye kilimo hususani cha mpunga hivyo ujio wa mwekezaji huyo mkoani hapa utasaidia kuongeza tija kwenye zao hilo.
Katika hatua nyingine baadhi ya wakulima wamesema kuwa ujio wa mwekezaji huyo utawasaidia wao kuzalisha kwa tija ikilinganishwa na awali," tukianza kulima kilimo cha umwagiliaji tunaamini tutavuna mavuno mengi maana tutalima zaidi ya mara moja kwa msimu" alisema Monika Msabila
"Kuna kipindi mavuno yanashuka kama mvua zikiwa chache sasa ujio wa mwekezaji huyu tumeupokea maana atatusaidia na sisi kulima kilimo cha umwagiliaji na kuacha kutegemea mvua pekee " alisema Simon Ngelela mkazi wa Kijiji cha Shigala wilayani Busega.
Katika hatua nyingine mwekezajI alipata fursa ya kutembelea kiwanda kinachomilikiwa na Mwekezaji mzawa, Deogratius Kumalija ambacho kinaongeza thamani kwenye mazao ya chakula hususani mpunga na mahindi Busega Mazao Limited kilichopo wilayani Busega.
MWISHO