Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI MABULA AZITAKA HALMASHAURI KUPANGA MIJI KUEPUKA MIGOGORO

Na Munir Shemweta, WANMM KIGOMA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amezitaka Halmashauri nchini kuhakikisha zinapanga, kupima na kumilikisha ardhi ili kuepuka migogoro ya ardhi pamoja na kuongeza mapato ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi.

Dkt Mabula alitoa agizo hilo jana mkoani Kigoma wakati akizungumza na watumishi wa sekta ya ardhi wa halmashauri nane za mkoa huo akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi. Halmashauri hizo ni Buhigwe, Kasulu DC, Kasulu TC, Kakonko, Kibondo, Kigoma DC, Kigoma MC, na Uvinza DC.

Alisema, wakurugenzi wa halmashauri wanapaswa kutambua kuwa wana jukumu la kusimsmia halmashauri zao ili ziwe na miji yenye mpangilio mzuri ambapo alibainisha kuwa kama maeneo ya miji hiyo yataachwa bila kupangwa, kupimwa na kumilikishwa basi yatakuwa hovyo na maeneo mengi kuingia kwenye zoezi la urasimishaji.

‘’ Halmashauri zote nchini jukumu la kupanga miji ni la kwenu Wizara itasimamia nidhamu na ajira na mkizubaa katika hili miji itaendelea kuwa mibaya na serikali haitaki kuona ujenzi holela ukiendelea’’ alisema Naibu Waziri Mabula.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, urasimishaji unaofanyika sasa katika maeneo mbalimbali umesababishwa na kasi ndogo ya upangaji miji unaofanywa na halmashauri na kinachofanyika katika zoezi hilo ni huruma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wananchi na kubainisha kuwa mwisho wa zoezi la urasimishaji ni mwaka 2023.

Alisema, hata idadi ndogo ya hati zilizotolewa katika halmashauri za mkoa wa Kigoma ni ishara ya kasi ndogo ya upangaji na upimaji katika mkoa wa Kigoma ambapo Naibu Waziri Mabula alishangazwa na halmashauri za Kigoma DC na Kasulu DC kwa kushindwa kutoa hata hati moja katika kipindi cha nusu mwaka huku halmashauri ya Buhigwe ikitoa hati sita tu na hivyo kuutaka mkoa kuhakikisha unazisimamia halmashauri hizo ili ziweze kupanga, kupima na kumilikisha maeneo mengi zaidi.

Kuhusu suala la mapato ya kodi yataokanayo na ardhi, Naibu Waziri Mabula ameoneshwa kutofurahishwa na kasi ya ukusanyaji mapato katika mkoa wa Kigoma ambapo kwa kipindi cha nusu mwaka 2019/2020 halmashauri za mkoa huo zimekusanya shilingi milioni 312,233,500.9 sawa na asilimia 13 tu huku Kigoma DC na Kasulu DC zikiwa zimekusanya mapato ya ardhi chini ya asilimia 1.2 na halmashauri pekee iliyofanya vizuri ni Kakonko iliyokusanya milioni 17,281,142.59 sawa na aslimia 28.

‘’Kama taasisi nyingine za serikali kama TRA zingekuwa hazikusanyi kodi kama ulivyo mkoa wa Kigoma katika suala la ardhi ambapo mna asilimia 13 tu basi miradi mikubwa inayofanywa kwa kutumia kodi za ndani ingekwama’’ alisema Dkt Mabula.

Awali Afisa Ardhi wa mkoa wa Kigoma Jairo Pilla katika taarifa yake ya nusu mwaka 2019/2020 ya utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Kigoma alisema, kiwango kidogo cha kodi ya ardhi kilichokusanywa kwenye mkoa wake kimesababishwa na sehemu kubwa ya ardhi kwenye mkoa huo kutopimwa na kumilikishwa.

Aidha, alisema suala lingine lilichongia mapato kidogo ya ardhi ni idara ya ardhi kutopewa kipaumbele na halmashauri za mkoa huo ambapo hakuna bajeti inayotengwa kwa ajili ya kupanga na kupima maeneo na kitu pekee kinachofanyika ni zoezi la urasimishaji na kusisitiza michoro mingi inayowasilishwa ni ya urasimishaji tu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com