Jeshi la Marekani limekiri kuanguka kwa Ndege yake moja ya kijeshi katika eneo la Deh Yak, jimbo la Ghazni huko Afghanistan lakini limekanusha vikali madai kwamba ndege hiyo imedunguliwa na Wapiganaji wa Taliban.
"Wakati tukiendelea na uchunguzi wa ajali hii, hadi sasa hakuna viashiria vyovyote vinavyoonesha kwamba ndege yetu iliangushwa kwa Kombora " Amesema msemaji wa Jeshi la Marekani Col. Sonny Leggett
Awali, Waziri wa Ulinzi wa Marekani alikataa kutoa maelezo kuhusiana na ndege ya nchi hiyo iliyoanguka nchini Afghanistan.
Mark Esper aliwaambia waandishi wa habari kwamba, anazo habari kuhusu tukio hilo lakini kwa sasa hawezi kutoa maelezo zaidi.
Duru za kuamininika zinasema kuwa, ndege hiyo ilikuwa aina ya Bombardier E-11A na kwamba ilikuwa ikiunganisha mawasiliano baina ya ndege zisizo na rubani za Marekani katika kanda hii.
Kijiji ambacho ndege hii imeanguka, kusini magharibi mwa mji mkuu Kabul, ni eneo lenye idadi kubwa ya kundi la Taliban.
Msemaji wa kundi la Taliban, Zabihullah Mujahid amesema kuwa, ndege hiyo iliyotunguliwa ilikuwa na askari wa Marekani waliokuwa katika operesheni ya ujasusi kwenye anga ya mkoa wa Ghazni.
Mujahid ameongeza kuwa, ndege hiyo imetunguliwa na wapiganaji wa Afghanistan na kwamba ilikuwa na maafisa kadhaa wa ngazi za juu wa shirika la ujasusi la Marakeni, CIA.
Taarifa iliyotolewa na kundi la Taliban imesema watu waliokuwemo katika ndege hiyo ya jeshi la magaidi wa Marekani wakiwemo maafisa wa CIA wameaga dunia