Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NIDA WAAGIZWA KUFANYA KAZI MASAA 16 ILI KUTIMIZA AGIZO LA RAIS MAGUFULI

Na Mwandishi Wetu

Katika kwenda sambamba na siku 20 zilizongezwa na Rais Dkt.John Magufuli wakati akisajili laini yake ya simu kwa alama za vidole Desemba 27,2019 mjini Chato mkoani Geita,Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA) wametakiwa kuongeza idadi ya watumishi katika kituo cha kuchakata taarifa za waombaji nchi nzima kilichopo Kibaha mkoani Pwani ili  kuhakikisha kila mwananchi anayekidhi vigezo kupata  Kitambulisho cha Taifa ili aweze kusajili  laini yake ya  simu.

Akizungumza baada ya kutembelea kituo hicho Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dkt. Anold Kihaule kuongeza idadi ya watumishi katika kituo hicho na kuongeza pia masaa ya kufanya kazi kutoka nane mpaka kumi na sita ili kuhakikisha wananchi wanapata namba na vitambulisho baada ya nyongeza ya siku 20 ziliyotolewa na Rais Magufuli.

“Nimetembea katika vituo mbalimbali vya NIDA nchi nzima,changamoto kubwa wanayotoa wananchi ni kwenda kila siku kufuatilia kitambulisho au namba katika kituo husika lakini wamekua wakipata majibu kwamba bado kipo kwenye mchakato,wakati mwingine ameomba miaka mitatu iliyopita sasa anapoteza muda na gharama kufuatilia kitambulisho lakini nimetembelea hapa leo nimegundua uchache wa watumishi,mkurugenzi ongeza watumishi hapa..” alisema Masauni

“……naomba pia ongeza muda wa kufanya kazi,kutoka masaa nane mpaka kumi na sita,Rais ashasema muda hautaongezwa wa usajili laini za simu,sasa wananchi wanafurika na kupata taabu vituoni huko,sisi ndio wawakilishi wao lazima tuwasemee na mkuu wa nchi ashatoa maelekezo sasa ni utekelezaji tu” aliongeza Masauni

Akizungumza katika ziara hiyo Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dkt. Anold Kihaule alisema watayatekeleza maagizo hayo ya serikali huku akiwaasa wananchi ambao tayari wana namba za utambulisho waende kusajili laini zao ili kwenda sambamba na muda ulioongezwa na Rais Dkt. Magufuli.

 “Jumla ya watu milioni 7.6 tayari wana namba za utambulisho nchi nzima na kila siku tunaendelea kutoa namba hizo sehemu mbalimbali nchini na mnaweza kuona kwa Dar es Salaam katika Viwanja vya Mnazi Mmoja tunatoa namba pale nani zoezi la siku zote za wiki,hatuna sikukuu wala siku za mwisho za wiki” alisema Dkt.Kihaule

Kila mmiliki wa simu ya mkononi anatakiwa kusajili laini yake kwa alama za vidole kwani kutofanya hivyo itamaanisha kutoweza kupiga wala kupokea simu,vile vile muhusika hatoweza kutuma wala kupokea ujumbe mfupi wa maneno.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com