Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

OFISA NIDA NA WAKALA USAJILI LAINI ZA SIMU MATATANI KWA KUOMBA FEDHA WANANCHI WAWAPE NAMBA ZA NIDA



Ofisa msajili msaidizi wa mamlaka ya vitambulisho vya taifa Nida Mkoani Shinyanga Haruna Mushi, pamoja na wakala wa usajili laini za simu za mkononi Victor Isack Vicent, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kutoza fedha wananchi kiasi cha Shilingi 30,000, ili wawapatie namba za Nida na kusajili laini zao za simu kwa alama za vidole.


Tukio hilo limetokea leo  Jumatatu Januari 20,2020 majira ya saa saba mchana wakati mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, alipofika kwenye ofisi za mamlaka ya vitambulisho vya taifa Nida Mjini Shinyanga baada ya kupata taarifa za wananchi kuombwa fedha ili wapate namba za Nida.

Akielezea tukio hilo mkuu huyo wa wilaya Mboneko, ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Shinyanga ,alisema wakati akiwa kwenye ofisi hizo za Nida, amepata taarifa za wananchi kuombwa pesa kutoka kwa wakala wa usajili la laini za simu za mkononi ambaye alikuwa akifanya mawasiliano na ofisa huyo wa Nida.

Alisema mara baada ya kumkamata wakala huyo wa usajili wa laini za simu za mkononi kwa alama ya vidole, walipomfikisha Polisi na kuanza kumhoji kwanini anatoza fedha wananchi ili awapatie namba za Nida, na wakati yeye siyo mtumishi wa Nida, ndipo akasema huwa anashirikiana na mmoja wa maofisa na Nida.

“Baada ya kumkamata wakala huyu wa usajili wa laini za simu za mkononi kwa alama za vidole, ndipo akamtaja Ofisa huyu wa Nida Haruna Mushi kuwa wanashirikiana naye kuomba fedha wananchi, ambapo yeye ndiyo mtoaji wa namba za Nida, na wakala huyu wa simu ndiyo mkusanyaji wa fedha,”alisema Mboneko.

“Tulipopewa taarifa hiyo ikabidi tumkamate na huyu Ofisa wa Nida Haruna Mushi, ambapo tumefanya uchunguzi wa simu zao na kubaini kuwepo na mawasiliano ya wananchi kuwaomba fedha na baadhi yao wameshatuma fedha hizo kwenye simu zao, ambapo bado tunaendelea na uchunguzi zaidi,”aliongeza.

Pia alitoa wito kwa wananchi wa Shinyanga kuacha tabia ya kutoa fedha ili kupata namba za vitambulisho hivyo vya taifa Nida kwani Serikali inatoa namba hizo bure, huku akiagiza maofisa wa Nida wafanye kazi usiku kucha na kutofunga ofisi hizo, hadi pale watakapo wamaliza watu wote kuwapatia namba hizo za Nida.

Kwa upande wakala huyo wa usajili wa laini za simu za mkononi kwa alama ya vidole Victor Isack Vicent, alikiri kufanya kazi hiyo ya kuomba fedha wananchi ili awasaidie kupata namba za Nida, kwa kushirikiana na ofisa huyo wa Nida Bwana Haruna Mushi, huku akiomba msamaha kwa kufanya makosa hayo.

Hata hivyo Ofisa huyo msajili msaidizi wa Nida mkoa wa Shinyanga Haruna Mushi, alikanusha tuhuma hizo za kushirikiana na wakala huyo wa usajili wa laini za simu za mkononi kwa alama ya vidole kuomba fedha wananchi, huku akikiri huwa anampatia majina ya watu kwa SMS na kisha kumuangalizia namba za Nida.

Kaimu kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Joseph Paulo, alisema kuwa upelelezi bado unaendelea ambapo wamewakabidhi Takukuru na ukikamilika watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.

TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI


Ofisa msajili msaidizi wa mamlaka ya vitambulisho vya taifa Nida mkoani Shinyanga Haruna Mushi (kushoto) akiwa mikononi mwa Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kutoza fedha wananchi Shilingi 30,000 ili awapatie namba za Nida akishirikiana na wakala wa usajili wa laini za simu kwa alama ya vidole Victor Isack Vicent.Picha zote na Marco Maduhu- Malunde 1 Blog
 
Ofisa msajili msaidizi wa mamlaka ya vitambulisho vya taifa Nida mkoani Shinyanga Haruna Mushi (kushoto) akiwa kwenye kituo cha Polisi wilaya ya Shinyanga kwa tuhuma za kutoza fedha wananchi Shilingi 30,000 ili awapatie namba za Nida akishirikiana na wakala wa usajili wa laini za simu kwa alama ya vidole Victor Isack Vicent (kulia)

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akitoa tahadhari kwa wananchi kuacha tabia ya kutoa fedha ili wapatiwe namba za vitambulisho vya taifa Nida, ikiwa namba hizo zinatolewa bure.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akiwataka wananchi wawe na uvumilivu na kuacha kutoa fedha ili kupata namba za Nida, ikiwa zoezi hilo litaendelea licha ya laini kuzimwa ili wananchi wote wapate namba za Nida na kusajili laini zao kwa alama ya vidole.

Wananchi wakiwa kwenye ofisi za Nida Shinyanga mjini wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko na kutakiwa kutotoa fedha yoyote ile ili wapate namba za Nida.

Wananchi wakiwa kwenye ofisi za Nida Shinyanga mjini wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko na kutakiwa kutotoa fedha yoyote ile ili wapate namba za Nida.

Picha zote na Marco Maduhu- Malunde 1 Blog


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com