Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo [CHADEMA]kanda ya kati,Lazaro Nyalandu amesema katika mwaka huu wa Uchaguzi mkuu,2020 Chama hicho kimejipanga kushinda na kuliongoza jiji la Dodoma.
Akizungumza leo Januari,12,2020 jijini Dodoma na Waandishi wa habari Mhe.Nyalandu amesema Kipaumbele cha CHADEMA kanda ya kati ni kuhakikisha jiji la Dodoma linakuwa mikononi mwa Chama hicho.
"Kipaumbe No 1 cha CHADEMA kanda ya kati ambapo mimi naongoza ni kuhakikisha tunaliongoza jiji la Dodoma,ambalo ni makao makuu ya nchi yetu kama ilivyo desturi ya CHADEMA ni kuchukua kwanza eneo ambalo watawala wamekaa.Kama mnakumbuka mwaka 2015 jiji la Dar Es Salaam lilichukuliwa na CHADEMA"amesema.
Aidha,ameendelea kusema "Tutashinda kwa mbinu zinazojulikana na mbinu zisizo julikana hivyo Wanachama tuhakikishe tunaipa raha CHADEMA"amesema.
Pia Mwenyekiti huyo wa CHADEMA kanda ya Kati amesema kuna uhitaji mkubwa wa kuwa na tume huru ya Uchaguzi hali itakayoipa heshima Kubwa nchi ya Tanzania na Kuisaidia CCM itakapokuwa Chama cha Upinzani.
"Kuna Msisitizo mkubwa sana ambapo pana uhitaji wa tume huru ya uchaguzi ,Demokrasia yetu itakuwa ya kuigwa Afrika Mashariki na ukanda wa SADC kwa ujumla"amesema.
Katika hatua nyingine Nyalandu amesema mchakato wa kurekebisha daftari la Mpiga kura lifanyike kwa ueledi kabla ya uchaguzi huku akiomba sheria ya vyama vya siasa kufanyiwa marekebisho hali itakayoruhusu wanasiasa na asasi za kiraia kuruhusiwa kushiriki kuhamasisha watu kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura huku pia akisisitiza vyombo vya Ulinzi na Usalama kutojihusisha na Masuala ya siasa.
Sanjari na hayo Nyalandu amesema CHADEMA sio chama cha kulalamika tu na kuwaomba wanaohusika na Masuala ya kilimo kuhakikisha wanasambaza pembejeo za kilimo katika kipindi hiki cha Mvua ili wakulima walime kwa wakati hali itakayosaidia kupata chakula cha kutosha.