Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akizungumza kwenye mkutano na wadau wa madini katika ukumbi wa Mount Meru jijini Arusha. |
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akipewa maelezo na mfanyabiashara wa madini katika soko la madini jijini Arusha. |
Balozi wa China nchini Tanzania Wang ke akizungumza kwenye mkutano na wadau wa madini katika ukumbi wa Mount Meru jijini Arusha |
Balozi wa China nchini Tanzania akikabidhiwa zawadi kutoka kwa mfanyabiashara wa Madini. |
NAIBU wa Madini Stanslaus Nyongo akitoa maelekezo kwa wafanyabiashara wa Madini jijini Arusha, mbele kulia ni Mwenyekiti wa Tume ya Madini Profesa Idris Kikula na wapili kutoka kushoto ni Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Arusha Mhandisi Khamis Kamando.
Na Tito Mselem Arusha,
Naibu
Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, ameonya tabia ya baadhi ya Vyombo
vya Ulinzi na Usalama kuwakamata wafanyabiashara wa madini wenye vibali
na wanaofata Sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali katika shughuli
hiyo.
Kauli hiyo ameitoa
Januari 15, jijini Arusha wakati akifungua Mkutano wa Mabalozi wa
Tanzania nchini China Mbelwa Kairuki na Balozi wa China nchini Tanzania
Wang Ke pamoja na wadau wa madini uliolenga kujadili fursa za biashara
katika sekta ya Madini.
“kumeibuka
tabia ya kuwakamata na kuwasumbua wafanyabiashara wa madini ambao wengi
wao wanavibali halali vya kumiliki madini hii ni kunyanyasa
wafanyabiashara wasio na hatia, tumefungua
masoko ya madini mikoani ili wafanyabiashara wetu wasinyanyasike”, alisema Nyongo.
Aidha, Nyongo, amewataka Polisi watakao kamata wafanyabiashara wakiwa na madini majumbani mwao, kuhakikisha wanawatumia Maofisa Madini ili kujua kama madini hayo yanavibali kwa kuwa sheria inaruhusu wafanyabiashara kukaa na madini ilimradi wanavibali na wafuate sheria.
Alisema ili kuondoa mkanganyiko huo, Wizara imejipanga kuelimisha wadau wa
madini vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu sheria za madini
ikiwemo inayoruhusu wafanyabiashara hao kushikilia madini kabla ya
kuyauza katika masoko ya madini.
Pia,
Nyongo aliwasisitiza Mabalozi wa China nchini Tanzania Wang Ke na yule
wa Tanzania nchini China Mbelwa Kairuki kuendelea kuhamasisha
wawekezaji kuwekeza nchini hususan kwenye masuala ya uongezaji thamani
madini chini ya gramu mbili ambayo yanaruhusiwa kwenda nje ya nchi
bila kuongezwa thamani.
"Kama
mnateknolojia ya kuongeza thamani madini haya tunawaalika mje kuwekeza
ili tusiyatoe nje bila kuongeza thamani,” alisema Nyongo.
Wakati
huo huo, Naibu Waziri Nyongo, amewahakikishia wawekezaji waliowekeza
katika Sekta ya Madini mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na
kuhakikisha anasimamia kuondoa kero mbalimbali zinazowakabili.
Awali,
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alisema mchango wa Sekta ya Madini
katika pato la taifa bado ni mdogo hivyo ipo haja kuendelea kuyatangaza
madini yetu na kushiriki maonyesho mbalimbali ya kimataifa.
Amesema
serikali imeamua kutumia balozi zake katika kutangaza madini
yanayopatikana hapa nchini ikiwemo madini adimu ya Tanzanite.
Aidha,
katika hatua nyingine Gambo, amewahakikishia wawekezaji kutoka China
waliowekeza katika Mkoa wa Arusha, mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja
na kuwaahidi kwamba atasimamia kuondoa kero na changamoto mbalimbali
zinazowakabili wawekezaji hao.
Alisema
nchi ya Tanzania ina madini mengi lakini mchango wake kwa pato la Taifa
ni asilimia 5.07 tofauti na pato la Sekta ya Utalii asilimia 17 na
asilimia 25 katika kulingizia Taifa fedha za kigeni.
"Mchango
huu hautoshi hivyo tumeamua kutumia mkutano huu ili tuongeze fursa
katika madini na kukuza zaidi pato la sekta hii," alisema Gambo.
Kuhusu
ukusanyaji wa maduhuli ya serikali Gambo alisema yanatokana na soko la
madini Namanga ambapo lilikusanya Shilingi bilioni 1.7 na soko la Arusha
limekusanya Shilingi bilioni 34.46 katika kipindi cha Juni 2019 hadi
Desemba 2019.
Naye,
balozi wa Tanzania Nchini China, Mbelwa Kairuki amewataka
wafanyabiashara wa madini nchini kujipanga kwa kutafuta viza mapema ili
kushiriki soko la madini nchini china linalotarajiwa kufanyika Novemba
10 hadi 15 mwaka huu.
"China
ni wanunuzi wakubwa wa dhahabu kama mwaka jana 2019 walinunua dhahabu
tani 1506 hiki sio kiwango kidogo na hata madini mengine wananunua sana
hivyo tujitahidi kuongeza fursa za soko nchini China,” alisema Kairuki.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Madini Profesa Idris Kikula amewataka
Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa yote nchini kukaa pamoja na vyombo vya
ulinzi na usalama kuelimishana kuhusu sheria za madini ili wawe na
namna bora ya pamoja ya kudhibiti utoroshaji wa madini nchini.
Social Plugin