Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAKUKURU SHINYANGA YAOKOA MIL. 30 KUTOKA KWA VIONGOZI WA AMCOS WALIOFANYA UBADHIRIFU WA FEDHA ZA WAKULIMA WA PAMBA


Na Josephine Charles - Malunde 1 blog
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Shinyanga imeokoa kiasi cha Shilingi 30,503,650 kutoka kwa Viongozi wa Vyama vya ushirika (AMCOS) waliofanya ubadhirifu wa Fedha za Wakulima wa Pamba msimu wa Mwaka 2018/2019.



Hayo yameelezwa leo Jumanne Januari 14,2020 na Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga ,Hussein Mussa wakati akizungumza na waandishi wa Habari katika ofisi za Taasisi hiyo kwa lengo la kutoa taarifa ya kazi zilizofanywa na TAKUKURU Shinyanga katika kipindi cha Robo ya Pili ya Mwaka wa Fedha 2019/2020 yaani kuanzia Oktoba hadi Desemba 2019.

Mussa amesema pamoja na kazi nyingine za kawaida za TAKUKURU ikiwemo Uchunguzi, Elimu kwa umma,kuzuia Rushwa,ufuatiliaji wa Miradi na kuendesha kesi zilizofunguliwa mahakamani kwa Makosa mbalimbali  ya Rushwa,TAKUKURU Shinyanga ilifuatilia kwa kina madeni ya Wakulima wa Pamba wanaodai fedha zao kutokana na pamba waliyouza kupitia AMCOS mbalimbali katika Mkoa wa Shinyanga. 

Ameeleza kuwa Baada ya uchunguzi TAKUKURU  ilibaini kuwa AMCOS saba kati ya zilizofuatiliwa ambazo ni Lugana, Mwakipoya, Ng'washinong'hela,Nyenze na Kalitu vya wilaya ya Kishapu,Kweli Balimi na Ibadakuli za wilaya ya Shinyanga ndizo zinadaiwa fedha na wakulima wa pamba kiasi cha shilingi 109,497,130/= fedha ambazo walizifanyia ubadhirifu kwa kutumia Fedha nyingi za wakulima zilizotolewa mwanzo na makampuni ya ununuzi wa Pamba kugharamia shughuli za uendeshaji wa chama tofauti na fedha za ushuru wanazodai kutoka kwa makampuni,hivyo kupelekea kuwa na madeni wanayodaiwa na wakulima wa pamba.

Amesema Takukuru ilibaini kuwa mpaka kufikia mwezi Desemba 2019 makampuni yaliyonunua pamba mkoani Shinyanga yalikuwa hayadaiwi Fedha za Wakulima bali walikuwa yanadaiwa ushuru wa AMCOS jumla ya Shilingi 890,105,580/= 

Ameeleza kuwa baada ya kubaini ubadhirifu huo Takukuru iliweza kuwakamata baadhi ya Viongozi wa AMCOS waliofanya ubadhirifu wa fedha za Wakulima na waliweza kurejesha kiasi cha Shilingi 30,503,650/= fedha ambazo zinategemewa kugaiwa kwa Wakulima hivi Karibuni.

Mussa amesema kwa viongozi wa AMCOS  ya Kweli Balimi ya Wilaya ya Shinyanga ambao walirejesha Fedha walizokuwa wanadaiwa kiasi cha Shilingi 6,362,400/= walizokuwa wamezifanyia ubadhirifu na tayari Fedha hizo zimekwisha gawiwa kwa Wakulima,hivyo Wakulima hawana madai wanayodai katika AMCOS hiyo.

Amewataka wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wametakiwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa  TAKUKURU kama ambavyo wamekuwa wakifanya ili Kuhakikisha wanaondoa Kero ya Rushwa katika mkoa wa Shinyanga. 
Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga , Hussein Mussa wakati akizungumza na waandishi wa Habari katika ofisi za Taasisi hiyo. Picha zote na Josephine Charles - Malunde 1 blog
Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Hussein Mussa wakati akizungumza na waandishi wa Habari katika ofisi za Taasisi hiyo.

 Shilingi 30,503,650 zilizookolewa kutoka kwa Viongozi wa Vyama vya ushirika (AMCOS) waliofanya ubadhirifu wa Fedha za Wakulima wa Pamba msimu wa Mwaka 2018/2019.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com