Na Ashura Jumapili - Malunde 1 blog Bukoba
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jn.Gaguti amelipongeza jeshi la polisi mkoa wa Kagera kwa jitihada zake katika kukabiliana na wahalifu na uhalifu katika mwaka 2019 ambapo hapakutokea tukio la unyang’anyi wa kutumia silaha licha ya mkoa huo kupakana na nchi tatu zenye changamoto ya kiusalama.
Brigedia Jen.Gaguti ametoa pongezi hizo katika hafla fupi ya kuwatunuku vyeti vya umahiri na ujasiri askari 19 wa jeshi la polisi Mkoani Kagera na wengine kutunukiwa vyeo mbalimbali kutoka vitengo tofauti ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao.
Alisema ukizingatia jiografia ya mkoa wa Kagera inapakana na nchi tatu ambazo zimekumbwa na changamoto za kiusalama lakini Kagera wamefanikiwa kudhibiti matukio ya kiuhalifu kwa mwaka 2019 hakuna matukio ya kutumia silaha yaliyotokea .
Aliwataka Askari wa jeshi hilo kukaza buti na kuacha kulegeza kwa mafanikio yaliyopatikana 2019.
Alisema Askari waliotunukiwa vyeti hivyo wameonekana kufanya vizuri Zaidi lakini kwa kuunga mkono jitihada za askari wengine katik uwajibikaji na ulinzi wa usalama wa mkoa ataanda hafla ya kuwapongeza wote mwezi huu.
Aidha,alisema anaridhishwa na nidhamu ya jeshi hilo kwa madai kuwa kama mkuu wa mkoa hajawahi kupokea malalamiko ya utovu wa nidhamu kutoka kwa askari wa jeshi hilo.
Awali akiongea katika hafla hiyo kamanda wa polisi Mkoani Kagera (ACP )Revocatus Malimi alisema mwezi Septemba ,2019 IGP Siiro,alipotembelea eneo la Nyakanazi Wilayani Biharamulo na Wilaya ya Ngara Mkoani humo katika ziara yake ya kikazi alipata fursa ya kuongea na askari ambapo aliridhishwa na utendaji kazi wao.
Alisema baada ya kuridhishwa na utendaji kazi wa askari hao hasa kitengo cha kupambana na majambazi hivyo akaamua kuwatunuku vyeti vya umahiri na ujasiri askari hao na wengine wakitunukiwa vyeo katika ngazi mbalimbali.
Alisema katika kuunga mkono jitihada za mkuu wa majeshi nchini ofisi ya RPC ,Kagera kupitia kumbukumbu mbalimbali za utendaji wa askari wamewatunuku Askari wengine vyeti hivyo na kiasi cha shilingi (50,000)kwa askari wote waliopata vyeti.
Social Plugin