RAIS MAGUFULI AMPA MAAGIZO MAZITO SIMBACHAWENE


Rais Magufuli amesema anahisi Wizara ya Mambo ya Ndani ina mapepo na kumtaka Waziri mpya wa wizara hiyo, George Simbachawene kuwa mkali, kumtanguliza Mungu mbele.



Magufuli ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Januari 27, 2020 Ikulu, Dar es Salaam baada ya kumuapisha Simbachawene, waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Azzan Zungu na mabalozi watatu.



Rais Magufuli amemtaka Simbachawene kubadili baadhi ya vitu katika wizara hiyo, kuwaondoa watendaji wasiofaa ili kuboresha utendaji.



“Nimekupeleka katika Wizara ambayo nahisi ina mapepo sasa mapepo hayo yasikuingie uwe mkali, usimamie, naamini utaweza na wakati mwingine umtangulize Mungu,” amesema Magufuli.

Amesema licha ya Simbachawene kupelekwa wizara ngumu, ugumu huo anaweza kuuleta mwenyewe.
 


Pia, amewataka watendaji serikalini kutoingia mikataba bila kuihusisha wizara ya Fedha na Mipango.

 “Hili la mkataba tumeshawaachia watu wa Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) sijui kama watafanya kazi vizuri au wataanza kuogopa ila nina uhakika hili watalifanyia kazi bila kujali nafasi za watu ili rasilimali hii ndogo iweze kutumika vizuri kwa ajili ya manufaa ya watu,” amesema.

Alimtahadharisha Simbachawene kuwa watendaji wote atakaowakuta katika wizara hiyo wanajua kuhusu suala hilo huku akimtaja naibu waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, “lakini (Masauni) hakuhusishwa sana ila alikuwa akipewa nakala ya madokezo na alikuwa ananyamaza hasemi serikalini.”

“Sifahamu kwa nini naye alikaa kimya lakini hakuhusika sana, Naibu katibu mkuu (Wizara ya Mambo ya Ndani) amehusika sana tangu kuanza kwake mpaka mwisho na una watendaji wengine katika Jeshi la Zimamoto wamehusika sana.”




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post