Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewatakia Watanzania wote heri ya Mwaka mpya wa 2020 na kuwaomba waendelee kudumisha amani na upendo ili uwe mwaka wa maendeleo na ustawi kwa Taifa.
Mhe. Rais Magufuli ametoa salamu hizo jana wakati akiagana na Maafisa na Askari Wanyamapori na Hifadhi ya Misitu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo ambako alitembelea na kujionea vivutio vya utalii pamoja na wananchi wa Nyabugera na Muganza aliowasalimu wakati akiwa njiani kurejea nyumbani kwake Chato Mkoani Geita.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amepokea salamu za heri ya Mwaka Mpya wa 2020 kutoka kwa wananchi, viongozi mbalimbali wakiwemo Marais Wastaafu, Maaskofu na Masheikh ambao wamempongeza kwa kazi nzuri ya kuongoza nchi kwa mafanikio makubwa na wamemuelezea matarajio yao ya kufanikiwa zaidi katika mwaka ujao.
“Mhe. Rais wangu, Dkt. Magufuli, Bwana Yesu Asifiwe. Ninakupa hongera sana kwa wajibu mzito ulionao. Kwa neema ya Mungu tumejaaliwa kufikia siku ya mwisho kwa mwaka huu wa 2019. Mimi nakupongeza kwa jitihada zako nyingi za kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Ninakuombea na kukutakia Mwaka Mpya 2020 wa heri na mafanikio makubwa. Uso wa Bwana uende nawe popote utakapokuwa” amesema Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dkt. Frederick Shoo.
Kabla ya kuondoka katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo, Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Dkt. Allan Kijazi, Maafisa na Askari wote wa hifadhi hiyo kwa mapokezi mazuri na juhudi kubwa zilizowezesha hifadhi hiyo kuvutia na amewahakikishia kuwa pamoja na kutoa shilingi Bilioni 2 za ujenzi wa kivuko cha kwenda hifadhi ya Kisiwa cha Rubondo, Serikali itatoa shilingi Milioni 200 za kuboresha barabara za hifadhi hiyo.
Baada ya kuvuka ziwa Victoria kwa kivuko cha MV Chato, Mhe. Rais Magufuli amekutana na wananchi wa Kasenda na kuelezea kutoridhishwa kwake na ukusanyaji wa mapato ya soko la dagaa na samaki la Kasenda baada ya kuelezwa kuwa makusanyo ya mapato ya soko hilo ni shilingi laki 5 kwa siku licha kuwa soko kubwa namba 2 kwa kuuza dagaa katika ukanda wa Ziwa Victoria.
Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Chato, kufuatilia ukusanyaji wa mapato katika soko hili na kuchukua hatua za kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato itakayobainika ili Halmashauri ya Wilaya ya Chato iweze kupata fedha zitakazosaidia kutatua kero za wananchi ikiwemo kuboresha mazingira ya soko hilo na ujenzi wa shule ya sekondari ya Nyabugera ambayo amechangia shilingi Milioni 5.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Bw. Eliud Mwaiteleke kutangaza zabuni ya ujenzi wa barabara ya Kasenda - Muganza yenye urefu wa kilometa 2.2 ili ijengwe kwa kiwango cha lami kama alivyoahidi, na kwamba Serikali itatoa fedha za ujenzi wa barabara hiyo.
Mhe. Rais Magufuli pia amewasalimu wananchi wa Muganza, ambapo amewapongeza kwa maendeleo yaliyopatikana katika eneo hilo na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma ili iendelee kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo yenye manufaa kwa wananchi.
“Nchi hii ilikuwa inaliwa sana na majizi na mpaka sasa bado wapo, namuomba Mwenyezi Mungu aendelee kunipa uhai ili katika mwaka 2020 niendelee kuwatumbua majizi wote na fedha tutakazopata tuzipeleke kwenye miradi ya maendeleo kama ambavyo tumenunua ndege 11, tunajenga reli (standard gauge), tunatoa elimu bure na mengine mengi” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli pia amemuonya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Bw. Eliud Mwaiteleke kwa matumizi mabaya ya fedha yanayofanywa na halmashauri hiyo na ametaka dosari hizo zirekebishwe mara moja. “Nataka ujirekebishe, wananchi hawa wanateseka sana” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
Social Plugin