Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAS SHINYANGA : VIONGOZI WA UMMA EPUKENI MIGONGANO YA KIMASLAHI KATIKA VITUO VYENU VYA KAZI

Na Salvatory Ntandu 

Mmomonyoko wa maadili na Migongano ya maslahi kwa Viongozi kwa baadhi ya viongozi wa mashirika na taasisi za Umma mkoani Shinyanga umetajwa kusababisha hasara kwa serikali kutokana na uwepo wa ufanisi mdogo  katika usimamizi wa miradi ya maendeleo.

Hayo yalibainishwa Januari 10 mwaka huu na Katibu Tawala wa mkoa wa Shinyanga Albert Msovela wakati akifungua mafunzo ya siku mmoja ya  sheria ya maadili yaliyofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kujumuisha watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya Umma.

Alisema kuwa  Sheria ya maadili ya Viongozi wa Umma inaelekeza majukumu ya viongozi wa taasisi na mashirika ya Umma, kusimamia sheria za Nchi, haki na utu ili kumsaidia Rais katika kutekeleza majukumu yake na hatimaye kutoa huduma bora kwa jamii na kuepuka kujiingiza katika migogoro isiyokuwana tija.

“Wapo  baadhi ya viongozi wa Umma wanaendekeza migogoro kwenye maeneo yao yakazi kwa kufanya kazi kwa makundi na kusababisha watumishi kutowajibika ipasavyo kinyume na viapo vyao,kama wapo humu hebu wajirekebisheni haraka kabla hatua za kinidhamu hazijachukuliwa dhidi yao, alisema Msovela.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kanda ya Magharibi inayojumisha mikoa ya Tabora,Shinyanga,Simiyu na Kigoma,kutoka Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma, Gerald Mwaitebele alisema kuwa endapo viongozi hao wataamua kubadilika malalamiko hayatajitokeza tena na wananchi watapata huduma za kijamii vizuri.

“Tangu tumeanza kutoa mafunzo haya katika mikoa yetu ya kanda ya magharibi tumeona mabadiliko makubwa hususani suala la maadili, uadilfu na vitendo vya rushwa limepungua na kutupa matumaini ya kuendelea kutoa elimu hii kwa ngazi zote kwenye jamii kama vile shuleni na kwenye mikutano ya hadhara ya vijji na mitaa” alisema Mwaitebele.

Nila Mabula ni Mshiriki wa Mafunzo hayo  ambaye pia ni Mkaguzi Mkuu wa ndani wa Mkoa, ameiomba Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma kutoa mafunzo hayo kwa watumishi wote wa umma ili kuzuia vitendo vya ukiukwaji wa maadili hususani pindi wanapokuwa wanatoa huduma kwenye jamii.

Mafunzo hayo yalijumuisha  Wakuu wa vyombo vya Usalama, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Makatibu Tawala wa Wilaya, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Idara na Vitengo, watendaji wa Mahakama na Wakuu wa Taasisi za Umma.

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com