RUGEMALIRA AFUNGUKA MAZITO MAHAKAMANI


Mfanyabiashara  James Rugemalira, amedai mahakamani kwamba ameandika barua kwenda kwa Kamishna  Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kumwelezea  namna benki ya Standard Chartered Hong Kong ilivyokuwa ikikwepa kodi na ushuru wa forodha. 



Mshtakiwa huyo na wenzake wawili wanakabiliwa na tuhuma za uhujumu uchumi ikiwamo kutakatisha fedha.

Rugemalira alitoa hoja hiyo jana Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi, wakati kesi hiyo ilipopangwa kwa ajili ya kutajwa.

Alitoa madai hayo baada ya Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Maghela Ndimbo, kudai kuwa kesi ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika.

Rugemalira aliomba ruhusa ya kuzungumza na aliporuhusiwa alidai kuwa Januari 24, mwaka huu, alizungumza na mwakilishi wa Takukuru alipotembelea mahabusu na akamkabidhi nakala ya barua hiyo aliyoandika kwenda kwa Kamishna Mkuu wa TRA lakini mpaka sasa hajapata majibu yake.

"Mheshimiwa Hakimu, naomba mahakama yako itakapopanga tarehe nyingine ya kutajwa, upande wa Jamhuri walete majibu kwa sababu wanaostahili kushtakiwa katika kesi hii ni benki hiyo lakini nashangaa kuona wengine wanaunganishwa kwa madai upelelezi haujakamilika.

"Mheshimiwa Hakimu upelelezi wa kesi hii hautakamilika. Kama kweli wanataka ukamilike, wafuatilie hiyo barua aliyowapelekea TRA,” alidai Rugemalira.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Shaidi alisema kesi hiyo itatajwa Februari 13, mwaka huu, na washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu.

Mbali na Rugemalira, washtakiwa wengine ni Harbinder Sethi na Joseph Makandege.

Katika kesi ya msingi ya uhujumu uchumi namba 27/2017, Makandege anakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuisababishia serikali hasara ya dola za Marekani 980,000 pamoja na utakatishaji wa Fedha.

Kwa upande wa Sethi na Rugemalira, walifikishwa mahakamani hapo zaidi ya miaka miwili na wamekaa rumande, kutokana na upelelezi wa kesi yao kutokukamilika.

Washitakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 12 yakiwamo ya utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27, kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani hapo Juni 19, 2017.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post