Na Amiri Kilagalila-Njombe
Serikali nchini Tanzania imejipanga kuja na mpango wa ujenzi wa viwanda vya kutengeneza mbolea nchini,ili kuondokana na tatizo la mbolea,kuwa na mbolea zinazofaa,zenye bei naafuu pamoja na mbolea zinazokidhi mahitaji ya udongo.
Hayo yamebainishwa na waziri wa kilimo Mh.Japhet Hasunga mara baada ya kukagua uwepo wa pembejeo za kilimo kwenye maghala ya wauzaji wa Pembejeo mjini Makambako mkoani Njombe.
“Mpango mkubwa wa kuondokana na tatizo la mbolea ili tuwe na mbolea zinazofaa,ili tuwe na mbolea zile zinazokidhi mahitaji ya udongo wetu,ili tuwe na mbolea zitakazokuwa na bei naafuu, mkazo tumeuweka kuhakikisha tunajenga viwanda vya kutengeneza mbolea hapa nchini”alisema Waziri Hasunga
Aidha amesema mpango mwingine wa serikali kwa sasa ni kuja na bei elekezi kwa aina zote za mbolea tofauti na sasa bei elekezi ikiwa kwa aina mbili pekee za mbolea.
“Bei elekezi haina mjadala,tulishatangaza bei elekezi mbolea za aina mbili,mbolea ya kupandia DAP na UREA ina bei elekezi,bei elekezi ni bei ya juu kabisa ambao tutawauzia mbolea kwa hiyo ina maana mawakala au makampuni wanatakiwa kuuza chini ya bei elekezi,kuna mbolea najua NPK,CAN,SA na zingine hazipo kwenye bei elekezi,lakini tunajipanga vizuri ili mwakani ikiwezekana tuje na bei elekezi kwa mbolea za aina zote”aliongeza Hasunga
Hasunga ameiagiza taasisi ya mamlaka ya usimamizi wa mbolea ndani ya siku saba kuhakikisha zinafikisha mbolea za aina zote hususani UREA mjini Makambako kwa kuwa eneo hilo ni kitovu cha kilimo kwa mikoa ya kusini.
“Nimeshudia kwamba mbolea zipo lakini hapa nimeona kuna upungufu wa UREA na sasa hivi ndio kipindi cha kuanza kutumia UREA kwa hiyo nimeagiza taasisi ya mamlaka ya usimamizi wa mbolea wahakiishe mbolea inafika Makambako sio zaidi ya siku saba”alisema tena Hasunga
Social Plugin