Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI NA WADAU WAKUTANA KUANDAA TAARIFA YA NCHI YA UTEKELEZAJI WA MKATABA WA KIMATAIFA WA KUTOKOMEZA AINA ZOTE ZA UBAGUZI DHIDI YA WANAWAKE

Na Mwandishi Wetu Morogoro
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bi. Regina Chonjo amewataka wadau wa haki na utetezi wa wanawake kuendeleza juhudi za Serikali ili kuhakikisha wanawake wanalindwa dhidi ya ubaguzi wa aina yoyote na kushiriki katika fursa za maendeleo na ustawi wao.

Bi. Chonjo alisema hayo wakati wa kuahirisha Kikao cha wadau wa Kitaifa waliokutana mjini Morogoro kwa lengo la kuboresha Taarifa ya Nchi ya Utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza aina zote za ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW).

Aidha Bi. Chonjo aliwapongeza wadau kwa kuweza kuainisha mafanikio yaliyofikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuzuia ubaguzi dhidi ya wanawake na wasichana kwa kipindi cha mwaka 2015 hadi 2019 akilitaja jambo hilo kuwa limetokana na utendaji wa pamoja.

’’Kazi hii ya kuandaa Taarifa ya Nchi ambayo mumeifanya kwa muda wa siku tatu itaboresha shughuli zilizofanyika na kuonesha jinsi Tanzania ilivyotekeleza masuala ya kutokomeza ubaguzi dhidi ya wanawake na pia kuwawezesha kiuchumi, kisiasa na kijamii’’. Aliongeza Bi. Chonjo.

Aidha Bi. Chonjo pia alisema idadi ya wanawake nchini Tanzania ni kubwa ukilinganisha na idadi ya wanaume uku akitaja takwimu zinaonesha kuwa kuna takriban asilimia 51 ya wanawake ukilinganisha na wanaume na kati ya hao 80% wanaishi vijijini wakijiajiri katika shughuli za kilimo, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuwalinda wanawake dhidi ya ubaguzi na aina zote za ukatili wa kijinsia ili kushiriki nafasi za maendeleo

’’Tukitambua kuwa idadi ya Wanawake nchini ni kubwa kwa asilimia 51 ukilinganisha na idadi ya wanaume hoja hii inakuwa msingi wa kuwekeza katika kukuza ushiriki wa wanawake ambapo takriban asilimia 80 ya wanawake hao wanaishi vijijini wakiwa wamejiajiri katika sekta ya kilimo, hivyo kuna uhitaji mkubwa wa kupinga ubaguzi dhidi ya wanawake’’.Alisisitiza kiongozi huyo wa Wilaya.

Aidha Bi. Chonjo alizitaja juhudi za serikali katika kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake  nni pamoja na kuanzisha Madawati ya Jinsia na Watoto 420 katika Vituo vya Polisi kwa lengo la kuwezesha kupata haki na huduma stahiki kwa wanawake na kuongeza kuwa  madawati haya yameongeza ari ya wananchi kujiamini na kuvunja ukimya katika utoaji taarifa za vitendo vya ukatili kwenye maeneo ya jamii.

Aidha Bi. Chonjo alivitaja Vituo vya pamoja vya  kutoa huduma kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia kuwa  vimeanzishwa katika mikoa sita ya Tanzania Bara ambavyo ni Dar es Salaam, Pwani, Mwanza, Mbeya, Iringa na Shinyanga vimewesha utoaji wa huduma stahiki kwa waathirika akivitaja kuwa hatua muhimu iliyochokuliwa na serikali kupambana na vitendo vya ukatili hapa Nchini.

Bi. Chonjo alitaja hatua nyingine iliyochukuliwa na Searikali kupuna na vitendo vya ukatili kuwa ni kufanya marekebisho ya Sheria ya Elimu na kulifanya kosa la kumpa mimba au kuoa au kuolewa mwanafunzi wa shule za msingi na sekondari kuwa kosa la jinai na pale inapothibitika adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 marekebisho haya yamesaidia kupunguza matukio ya mimba za utotoni.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia Bibi Mboni Mgaza ameeleza kuwa Taarifa hii ya Tisa ya Utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza aina zote za ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW)itawasilishwa Umoja wa Mataifa Mwezi Machi 2020 ikiwa imeunganisha taarifa ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.


                                              ---Mwisho.---


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com