Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YA TANZANIA YATENGA MAENEO MAALUM KUTIBU VIRUSI VYA CORONA


Waziri ya Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema mtu yeyote atakayepata virusi vya Corona nchini atatibiwa katika maeneo yaliyotengwa yaliyopo mkoani Kilimanjaro, Dar es Salaam na Mwanza.


Mlipuko wa virusi hivyo ulioanzia China hadi jana watu 106 wameripotiwa kufariki dunia huku zaidi ya 4,000 wakiambukizwa.

Akizungumza mjini Dodoma leo Jumatano Januari 29, 2020 Ummy amesema maeneo hayo ni Mawenzi (Kilimanjaro), Buswelu (Mwanza) na Kigamboni (Dar es Salaam) akaongeza kwamba   wizara inaendelea kujiandaa kukabiliana na tishio la ugonjwa huu endapo utaingia nchini.

“Tutahakikisha tunapata vifaa kinga, dawa na vifaa tiba vya kutosha,” amesema  na kufafanua kwamba watumishi wa wizara yake wanafanya uchunguzi kwa wasafiri wote kutoka Bara la Asia, kwenye mipaka na wanaoingia nchini kupitia viwanja wa ndege vilivyopo Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza.

Aidha amesema wanafanya uchunguzi katika bandari ya Dar es Salaam, ambapo wiki mbili zilizopita waliwachunguza watu 1,520 walioingia nchini kutokea China kupitia bandari hiyo na waliotumia mipaka mbalimbali na viwanja vya ndege.

Kwa mujibu wake,  wizara inavyo vipimajoto 140 (vya mkono 125 na vya kupima watu wengi kwa mpigo 15 ) vilivyofungwa kwenye mipaka. 

“Kutokana na mwenendo na kasi ya kusambaa kwa ugonjwa huu wa mapafu kipindi hiki, wizara inashauri kusubiri na kuepuka safari zisizo za lazima kwenda maeneo yaliyoathirika na inapolazimu kusafiri,  wapate maelezo ya kitaalamu kabla ya kuondoka nchini.

“Mpaka sasa Tanzania haina mgonjwa wala anayehisiwa kuwa na ugonjwa wa homa ya mapafu (Corona). Hata hivyo, kutokana na muingiliano uliopo kibiashara na kijamii kati ya Tanzania na nchi za Asia ikiwemo China, nchi yetu inakuwa katika hatari ya ugonjwa huo,” amesema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com